Header Ads

Mkurugenzi Maswa Afariki Dunia Ghafla Kabla ya Ziara ya Waziri Mkuu.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekatisha ziara yake ya siku sita mkoani Simiyu, baada ya kifo cha ghafla  cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa (DED), Trasias Kagenzi kilichotokea juzi usiku.

Kaimu Katibu Tawala, Donatus Weginah alithibitisha kutokea kifo cha mkurugenzi huyo wakati Waziri Mkuu akiwa na ratiba ya kutembelea wilaya hiyo.

Weginah alisema juzi asubuhi Kagenzi alikuwa akifanya mazoezi ya kukimbia akiwa na mlinzi wake na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Rosemary Kirigini lakini alianza kujisikia vibaya.

“Mkurugenzi alikuwa akifanya mazoezi ‘jogging’ na DC Rosemary Kirigini, lakini baadaye alimwambia Kirigini najisikia pumzi zinabana, akamwambia aendelee… lakini mara mkuu wa wilaya alimuona amejiinamia, aliporudi kumuuliza akamwambia naona nakosa hewa, ndipo alipoamua kukimbia kuchukua gari kumpeleka hospitalini,”alisema.

Weginah alisema mkurugenzi huyo alipelekwa hospitali na majira ya saa tano asubuhi alionekana akiendelea vizuri, hata hivyo baadaye hali ikabadilika mchana na waliamua kumpeleka katika Hospitali ya Bugando kwa uchunguzi zaidi, lakini usiku wa saa saba alifariki dunia.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Tawala huyo, alisema mkurugenzi ana kama mwaka mmoja na nusu tangu alipohamia wilayani humo na kwamba familia yake iko Arusha.

Weginah alisema jana mchana mwili wa Kagenzi ulichukuliwa hospitalini Bugando na kuletwa wilayani Maswa ambapo leo asubuhi Waziri Mkuu Majaliwa ataongoza kuaga mwili wa mkurugenzi huyo, lakini baadaye wataangalia familia inaamuaje maana ilikuwa imebaki Arusha, kisha mambo mengine yatafuata.

No comments