Header Ads

Mkuu wa Mkoa Mwanza aigomea Mwauwasa Kuongeza Bei Ya Maji.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amepinga hatua za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) kuongeza bei ya maji kwa madai ongezeko hilo litasababisha wananchi wengi kukosa huduma.

Mulongo alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mwauwasa, namna wanavyotoa huduma kwa wananchi, changamoto zinazowakabili pamoja na mafanikio ya mamlaka hiyo.

Hivi karibuni Mwauwasa, ilitangaza kuomba kuongeza bei ya maji kwa kile ilichodai kupanda kwa gharama za mita za maji hivyo wanapendekeza kuongeza bei ya maji kitendo ambacho wananchi wengi jijini hapa walikipinga.

Mulongo akizungumza na wafanyakazi hao amesema kuwa katika ufuatiliaji alioufanya amebaini kwamba kuna mchezo uliandaliwa na mamlaka hiyo kwa lengo la kujinufaisha wao wenyewe na sio wananchi hivyo haungi mkono hatua hizo.

“Mimi ninafahamu kwamba hawa watu ambao mliwaleta na wakakubaliana na nyie kuongeza bei ya maji ni wa kwenu ambao mliwaaandaa ili kuwaaminisha wananchi, sasa suala hilo siliungi mkono.

“Utaratibu wa kuongeza bei ya maji ambao nyie mnadai kupanda kwa gharama za mita za maji kaeni muangalie upya namna ambayo mtafanya,” amesema Mulongo.

Hata hivyo Mulongo aliwataka wafanyakazi hao kuwajibika kwani ni wajibu wao kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi hususani wanaoishi katika maeneo ya miinuko.

No comments