Mgombea ubunge wa ACT Arusha Mjini amwombea kura Lowassa
Wakati waswahili wanasema adui yako mwombee njaa, msemo huo umekuwa tofauti kwa upande wa mgombea ubunge wa ACT - Wazalendo Jimbo la Arusha Mjini, Estomih Malla baada ya jana kupanda jukwaani na kumwombea kura za ndiyo mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Mgombea huyo alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliokuwa na lengo la kunadi pia sera na kumwombea kura mgombea wa chama chake, Anna Mnghwira, katika Uwanja wa Stendi Kubwa, mkoani Arusha.
“Jamani naombeni mtambue kuwa mimi ni msomi ambaye nina shahada (Hakuitaja ni ya nini), kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikitumia elimu yangu kwa faida ya familia yangu tu baada ya kufukuzwa udiwani na Chadema, sasa naombeni mnichague ili niitumie pia kuwatumikia kwa kuwaletea maendeleo yaliyoshindikana kupatikana kwa miaka mitano,”alisema.
Mgombea huyo, alisema maendeleo ya kweli yanaletwa na watu wa kweli na wazalendo. “Mimi ni mkweli, nipeni ridhaa ya kuwaongoza na msisahau kumpa ridhaa ya kuwa rais mheshimiwa Edward Lowassa, naamini hamtajutia kura zenu,” alisema Malla.
Alipoulizwa baada ya kumaliza mkutano wake kwa nini amemnadi Lowassa badala ya mgombea urais wa chama chake, Malla hakutaka kujibu bali alipanda gari lake na kuondoka.
Post a Comment