MBOWE AKATA RUFAA MAHAKAMA KUU DHIDI YA HUKUMU YAKE.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe amekata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yake Julai, mwaka huu, na kumtoza faini ya Sh1 milioni baada ya kupatikana na hatia katika kosa la jinai.
Mbowe alitozwa faini ya Sh1 milioni au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kumshambulia mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu wa 2010 katika Wilaya ya Hai, Nassir Yamin.
Hata hivyo, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Mbunge wa Hai, alilipa faini hiyo na kuachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Hai.
Katika rufaa hiyo namba 33/2015, iliyofunguliwa na wakili Peter Kibatala, Mbowe anailalamikia mahakama iliyomtia hatiani kuwa ilishindwa kushughulikia hoja muhimu katika kufikia uamuzi huo.
Pia, Mbowe analalamika kuwa mahakama ilishindwa kupima ushahidi kwa usahihi na pia, ilishindwa kutilia maanani ushahidi wa mashahidi wa upande wa utetezi akiwamo yeye.
Mbowe analalamika kuwa mahakama ilishindwa kutumia msingi wa jukumu la kuthibitisha shitaka pale ilipoeleza kuwa mashahidi wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi uliojitosheleza.
Kwa mujibu wa Mbowe, Mahakama hiyo ilitakiwa itumie dhana ya upande wa mashtaka kuwa unatakiwa uthibitishe shtaka bila kuacha mashaka, jambo ambalo halikufanyika.
Mkata rufaa huyo anailalamika pia mahakama hiyo ilishindwa kueleza sababu zilizoifanya ifikie uamuzi wake huo kama inavyoelekezwa katika sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Kutokana na sababu hizo, Mbowe ameiomba Mahakama Kuu kuifuta hukumu iliyomtia hatiani, kurejeshewa Sh1 milioni alizolipa kama faini na apewe nafuu nyingine yoyote ambayo mahakama itaona inafaa.
Rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa Septemba 2, mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari.
Post a Comment