Mtuhumiwa kinara mauaji ya polisi.
Kinara, Selemani Shabani Ulatule.
Makongoro Oging’ na Issa Mnaly, Mkuranga,GPL
WAKATI jeshi la polisi nchini likiendelea kuwasaka watuhumiwa wa mauaji ya polisi na kupora silaha katika Kituo cha Stakishari, Ilala jijini Dar, Uwazi limefanikiwa kuipata picha ambayo inadaiwa ni ya mtuhumiwa kinara wa tukio hilo aliyetajwa kwa jina la Seleman Shaban Ulatule.
ENEO LA TUKIO
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wanahabari wetu walifika katika Kijiji cha Mandikongo, Mkuranga, Pwani na wakazi wa maeneo ya jirani wakiwa katika hofu baada ya watuhumiwa hao waliokuwa wakiishi jirani na kijiji hicho kutoweka.
NGOME YAO YATEKETEZWA
Wanahabari wetu walioambatana na afisa mtendaji wa Kijiji cha Mandikongo, polisi na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), walishuhudia makazi ya watu hao yakiwa yameteketezwa kwa moto na wananchi wenye hasira kali.
WANANCHI WAZUNGUMZA
Wakizungumzia tukio hilo, wakazi wa kijiji hicho walisema majambazi hao waliokuwa wamejitenga na makazi ya wanakijiji, walitoweka na familia zao baada ya kupata taarifa kuwa kuna msako mkali unaofanywa na jeshi la polisi ambao ulifanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa, bunduki 15 za kivita na fedha zaidi ya shilingi milioni 170.
WALIVYOFICHA FEDHA
Wakizidi kuelezea tukio hilo, wakazi hao waliwaonesha waandishi wetu shimo ambalo walilitumia kuhifadhia fedha hizo ambapo juu yake waliweka kinyesi cha binadamu kilichokadiriwa kuwa ni cha watu saba ikiwa ni alama yao ambayo pia itamfanya mtu akisogelea eneo hilo alipitie mbali kwa kuona kinyaa.
“Tunaomba vyombo vya usalama kuhakikisha watuhumiwa wote wanapatikana na silaha nzito walizokimbia nazo maana wanaweza kuja kukivamia kijiji hiki na kufanya unyama wa kutisha pindi vikosi vya usalama vitakapoondoka hapa,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyeomba hifadhi ya jina lake gazetini.
MTENDAJI AZUNGUMZA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Issa Said Mchalaganga aliwataja watuhumiwa ambao walikuwa wakiongozwa na kinara wao Seleman Shaban Ulatule ni pamoja na Said Mohamed Ulatule, Ally Mohamed Ulatule, Hamis Mohamed Ulatule, Haji Seleman Ulatule na Ally Said Ulatule.
“Hao wote walikimbia nyumba zao na baadaye kuharibiwa na wananchi kwa kuteketezwa kwa moto,” alisema Mchalaganga.
WALIOKAMATWA
“Katika msako wa vyombo vya usalama walifanikiwa kumkamata Ramadhani Hamis Ulatule na mwenyekiti wa kijiji, Ramadhani Mohamed Ulatule kwa ajili ya mahojiano na kwa kweli tunampongeza Kamishna Suleiman Kova na vyombo vya usalama kwa kazi nzuri ya kubaini kikundi hiki na kufanikiwa kupata baadhi ya silaha,” alisema mtendaji huyo.
MAISHA YAO KIJIJINI HAPO
Wananchi wa kijiji hicho waliliambia Uwazi kuwa, watu hao ambao wanadaiwa kuwa majambazi kabla ya kubainika, walikuwa wakiishi maisha ya usiri na wakifanya mafunzo ya kijeshi porini.
WALIJITENGA NA SERIKALI
“Hawakupenda kushiriki na wanakijiji katika shughuli za maendeleo, upigaji kura, uhesabuji wa watu hata hospitali ya hapa walikuwa hawaji kupata huduma na haikujulikana walikokuwa wakipatia matibabu,” alisema mwanakijiji mmoja.
YADAIWA KUNA ASKARI ALIYEKUWA AKIWATEMBELEA
Wananchi wa kijiji hicho walidai kuwa, kulikuwa na askari mmoja wa Gereza la Dondwe lililopo karibu na kijiji hicho ambaye alikuwa rafiki wa majambazi hao aliyekuwa akiwatembelea mara kwa mara katika makazi yao.
“Huyo askari tulikuwa tunamuona akienda huko porini mara kwa mara sasa tangu tukio litokee hajaonekana, tunaiomba serikali imfuatilie,” alisema mkazi mwingine wa kijiji hicho.
WALIKATAA KUHESABIWA
Afisa mtendaji wa kijiji hicho aliwaeleza waandishi wetu kuwa walimtilia shaka kiongozi wa ukoo wa Ulatule, Seleman Shaban ambaye aliwahi kuandikiwa barua na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga yenye kumbukumbu namba AB/226/290/1/40 ya Agosti 31, mwaka 2012 (nakala tunayo) ikimhoji kwa nini aliwakataza watu wa eneo lake kuhesabiwa kwenye sensa.
“Hapo ndipo tulipotilia shaka haswa baada ya tukio hili kutokea. Seleman alikuwa hataki kabisa kujihusisha na shughuli za serikali. Hata wakati wa zoezi la sensa aliwakataza watu wa eneo lake kuhesabiwa,” alisema mtendaji huyo.
WALIISHI NA RAIA WA KIGENI
Uchunguzi unaonesha kwamba watu hao hawakupenda wananchi kutembelea wala kukatisha katika makazi yao na kulikuwa na nyumba nyingine jirani ambazo zinadaiwa walikuwa wakiishi watu wasio Watanzania.
SABABU YA KUVAMIA VITUO VYA POLISI NI NINI?
Inadaiwa kuwa kuna majambazi wana mpango wa kuanzisha kikosi kikubwa kama jeshi la kupambana na dola ambayo imewashikilia wafuasi wao katika magereza mbalimbali nchini.
Imeelezwa kwamba, utaratibu huo ulikwepo tangu zamani na walikuwa wakipata silaha za kivita kutoka kwa wakimbizi wa nchi jirani lakini hali hiyo ikadhibitiwa na serikali kukawa hakuna silaha inayoingia nchini kinyume na taratibu.
WABADILI MBINU
Inasemekana kwamba baada ya kuwa na uhaba wa silaha wakawa wanawavamia polisi katika vituo, mabenki na popote pale wanapofanyia doria wakiwa na silaha kisha kuwapora.
Uchunguzi mwingine unaonesha kwamba walioua katika Kituo cha Polisi Stakishari ni baadhi ya kikosi chao na baada ya kufanya mauaji walipitia Barabara ya Nyerere na kuingia Banana kuelekea Kitunda, Msongola, Mbande kisha kuingia katika pori la Kijiji cha Mandikongo.
Kamishna Kova alipoulizwa kuhusu mzee Ulatule na sakata zima la kambi hiyo ya watu hao waliotoroka alisema, suala hilo atalizungumzia Ijumaa kwa sababu ndiyo siku aliyopanga kuzungumza na waandishi wa habari.
“Siku hiyo ndiyo niliyopanga kuzungumza na waandishi wa habari hivyo uje na swali hilo nitalijibu,” alisema.
TUJIKUMBUSHE
Julai 12, mwaka huu watu wanaokadiriwa 16 walifanya uvamizi katika Kituo cha Polisi Stakishari na kuua polisi wanne na raia watatu kisha kupora silaha zaidi ya 24 ambapo Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP Lucas Mkondya waliapa kuwakamata watuhumiwa hao na silaha walizoiba.
Msako wa polisi katika ngome hiyo iliyokuwa jirani na Kijiji cha Mandikongo, polisi walifanikiwa kupata bunduki 15 ambazo baadhi ni zile zilizoporwa katika Kituo cha Stakishari.
Post a Comment