Header Ads

KIPA WA IVORY COAST ATUA AZAM.

KIPA Angban Vincent de Paul amewasili jijini Dar es Salaam juzi na jana amefanya mazoezi mepesi kwenye ufukwe wa Coco, Dar es Salaam akiwa na kikosi cha mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC.
Kipa huyo raia wa Ivory Coast ametua kwa klabu hiyo yenye makazi yake Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ili kufanyiwa majaribio kwa nia ya kusajiliwa.
Jana, alifanya mazoezi mepesi pamoja na beki raia wa nchi hiyo, Serge Wawa wakati wenzake wakijinoa vilivyo chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall.
Angban amekuja Azam FC kwa ajili ya kusaini mkataba wa kujiunga na timu hiyo baada ya kuwepo kwa mazungumzo kabla ya kutua nchini.
Kipa huyo ambaye ametokea Klabu ya Jeunesse ambayo inashiriki Ligi Kuu ya kwao, aliwasili juzi na wachezaji wengine wawili wa Azam FC raia wa Ivory Coast, beki Serge na mshambuliaji Kipre Tchetche.
Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, Hall alisema anashukuru ujio wa kipa huyo na kusema kabla ya kusaini itabidi awe amefanya majaribio ili kujiridhisha na kiwango chake.
“Ni kweli amekuja Azam ila yupo kwa majaribio endapo atafuzu basi atasaini mkataba ili aanze kutumikia klabu,” alisema Hall aliyerejeshwa kwa mara ya pili kuinoa timu baada ya kufukuzwa kwa Joseph Omog wa Cameroon kabla ya kumalizika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.
Katika mazoezi ya jana, Angban, Wawa na Kipre Tchetche walifan ya mazoezi yao pekee kwa vile walichelewa, ili kutafuta kasi ya kuendana na wenzao ambao walishaanza mazoezi mwezi mmoja uliopita.
Azam FC inamchukua kipa huyo kwa lengo la kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Afrika, kwani mwakani itacheza Kombe la Shirikisho.
Endapo atasaini Azam FC, kipa huyo atakwenda kugombea namba na makipa wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ali.
Usajili wake ukikamilika, Azam itakuwa na wachezaji wanne kutoka Ivory Coast, akitanguliwa na pacha Kipre Herman Tchetche na Kipre Michael Balou pamoja na Serge.
Angban alizaliwa Februari 2, 1985 mjini Anyama, Ivory Coast, na amewahi kudakia timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika fainali za Afrika zilizofanyika Benin mwaka 2005 na pia aliiwakilisha nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
Amewahi kudakia timu ya Taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN, ikiwemo ile ya mwaka 2009 ambayo Tanzania ilicheza nao na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Mrisho Ngassa, langoni akiwa yeye.

Angban aliibukia katika klabu ya vijana ya Rio Sport d’Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, na timu za Sewe Sports, ASEC Mimosas kabla ya kwenda kuchezea timu ya vijana ya Chelsea chini ya U-20.

No comments