KILA LA HERI WABUNGE WA TZ.
BUNGE la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linamaliza muda wake wa kikatiba leo kwa kuvunjwa na Rais Jakaya Kikwete mjini Dodoma baada ya kudumu kwa takriban miaka mitano.
Leo itakuwa siku ya mwisho kwa wabunge kadhaa kuwapo mjini Dodoma wakiwa na wadhifa huo wa uwakilishi wa wananchi, kwani wote sasa wanalazimika kwenda majimboni kutetea nafasi hizo.
Ni kipindi kigumu ndani ya mioyo ya wengi lakini kwa wanaofahamu kwamba cheo ni dhamana, hiki ni kipindi muhimu kwao kujipima iwapo wamefanikiwa kuwatumikia ipasavyo wananchi.
Bunge hili lililokuwa chini ya uongozi wa Mama Anna Makinda, lilizinduliwa Novemba 18, 2010 na kwa miaka hii inayokaribia mitano kuna mambo kadhaa mema na muhimu limeyafanya.
Kuna maazimio, uamuzi na sheria kadhaa muhimu kwa taifa zilitungwa, kufikiwa au kuamuliwa kwa pamoja kwa manufaa ya wananchi wote, jambo ambalo linastahili pongeze.
Kuna nyakati wabunge walisimama pamoja kama wawakilishi wa wananchi na kuungana kufikia maafikiano mema kabisa kwa mustakabali wa taifa, ingawa pia kulikuwapo na nyakati za mifarakano.
Wabunge wa upinzani waliianza safari ya Bunge la 10 wakiwa katika msukosuko mkubwa wa namna ya kuunda Kambi ya Upinzani Bungeni, lakini wamemaliza safari hiyo wakiwa wamoja ndani ya Ukawa.
Bunge hili linavunjwa bila kuwapo wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani baada ya kutokubaliana na mambo kadhaa ndani ya Bunge hilo wiki iliyopita, hivyo kutia doa demokrasia yetu.
Pamoja na hayo, tunaamini kuwa Bunge la 10 limejitahidi kusaidia kuwapo kwa amani na utulivu nchini hadi leo, miezi takriban mitatu tu kabla ya kundwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano.
Ndio maana tunachukua fursa hii kuwatakia kila lililo la kheri wabunge hawa katika safari yao ya kwenda kuomba ridhaa ya wananchi waweze kurejea tena Dodoma, tukiwashukuru kwa michango yao iliyoliwezesha taifa letu kuwa tulivu na salama hadi leo.
Post a Comment