KIKWETE KUHUTUBIA BUNGE LEO.
BUNGE la 10 linamaliza shughuli zake leo kabla ya Rais Jakaya Kikwete kulihutubia na kulivunja mjini hapa. Rais atahutubia Bunge hilo saa 10:00 jioni baada ya kukagua gwaride la heshima, lililoandaliwa na Jeshi la Polisi katika viwanja vya Bunge mjini hapa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge jana baada ya kukagua gwaride, Rais Kikwete atakwenda ukumbi maalumu wa Spika, kusaini kitabu cha wageni kabla ya kuingia ukumbini na kuhutubia.
Anatarajiwa kutoka katika ukumbi huo wa bunge saa 12:15 jioni, baada ya kuhitimisha shughuli za bunge hilo. Miongoni mwa viongozi watakaohudhuria shughuli hizo ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Gharib Mohammed Bilal na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Wengine ni marais wastaafu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mohammed Chande Othman.
Wakati Bunge hilo likifika ukomo wake, wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesusa kuhudhuria kikao cha leo wakati Rais atakapohutubia kwa mara ya mwisho.
Wabunge hao walifikia uamuzi huo kwa madai kuwa Serikali imepitisha miswada mitatu ya sheria, inayohusu petroli na gesi, kinyume cha kanuni.
Wakipinga upitishwaji wa miswada hiyo, wabunge hao wa upinzani walifanya vurugu zilizosababisha wabunge 35 kusimamishwa kuhudhuria vikao kuanzia viwili hadi vyote vilivyosalia.
Adhabu hizo zilitolewa na Kamati ya Maadili ya Bunge na uamuzi wa Spika kutumia mamlaka yake. Wakati Chadema ni miongoni mwa wana Ukawa, ambao leo hawahudhurii kuvunjwa kwa bunge hili, vile vile wakati Bunge likizinduliwa Novemba 2010, wabunge wa chama hicho pia walisusa kwa madai ya kutomtambua rais, ingawa baadaye walitengua msimamo huo.HABARI LEO.
Post a Comment