WANANCHI WALIA NA MKANDARASI WA BARABARA GEITA
Barabara inayotoka amerikani Chips Kuelekea Jimboni ikiwa kwenye hatua za awali za ujenzi. |
Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi akisisitiza suala la mkandarasi kushindwa kutekeleza ujenzi wa Barabara kwa wakati. |
Baadhi ya maeneo ambayo wananchi wameendelea kulalamika kuathiriwa na mvua kutokana na kifusi ambacho kimewekwa na mkandarasi kwenye Barabara ya Amerikani Chips inayoenda Jimboni. |
Bi,Getruda Daud ambaye ni mkazi wa Katundu akilalamika namna ambavyo wameendelea kupata shida kutokana na kushindwa kukamilika kwa ujenzi wa Barabara pamoja na daraja. |
Baadhi ya wananchi wakiangaika kuvuka kwenye kidaraja kidogo kutokana na kushindwa kukamilika kwa Daraja. |
Nyumba ikiwa imeenea maji kutokana na kifusi ambacho kimelalamikiwa na wananchi.
Na,Joel Maduka,Geita
|
Wananchi waishio Mtaa wa Katundu Kata ya Kalangalala Mkoani Geita wamemlalamikia mkandarasi ambaye anajenga Barabara ya Kilomita 1.2 inayotoka Amerikani Chips kuelekea Jimboni kuweka kifusi cha mchanga hali ambayo imekuwa ikisababisha maji kuelekea kwenye makazi yao pindi mvua zinaponyesha.
Mkandarasi huyo ambaye anajulikana kwa jina la Nyakiling’ani Constraction Limited(NCL) anatekeleza mradi huo kwa ufadhili wa Benki ya dunia na kusimamiwa na halmashauri ya Mji wa Geita.
Akizungumza na Mtandao huu,Bi,Getruda Daudi alisema wameendelea kupata shida kubwa kutokana na mkandarasi huyo kuweka kifusi na pindi wanapomwambia amekuwa akiwaambia hana gharama za kukitoa kifusi hicho.
“Mvua zikinyesha tumekuwa tukipata shida sanaa jamani yaani maji yote yanakuja kwenye nyumba zetu na sababu ni hiki kifusi ambacho mkandarasi amegoma kukitoa tumekwisha mwambia hadi na diwani wetu lakini alikuja akapiga picha akaondoka na sisi ndio tunaopata shida ila tunaona yuko kimya hatujui tufanyeje”Alisema Bi ,Getruda.
Bw, Nzugila Mazoya yeye amelalamikia kitendo cha mkandarasi wa eneo hilo kuchukua muda mrefu bila ya kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo pamoja na daraja hali ambayo kwa sasa imekuwa ikiwapa shida kwa kuzunguka umbali mrefu kutokana na njia kuzibwa.
Sanjari na hayo baadhi ya wafanyakazi ambao wanafanyakazi na Kampuni hiyo akiwemo Lanslaus Joseph na Majura Mfungo wamelalamikia kutokulipwa mishahara kwa muda mrefu sasa na pindi wanapomuuliza msimamizi amekuwa akiwasisitiza kufanya kazi kwa madai kuwa pesa itakuja na kwamba hawaoni jitihada ambazo zinafanyika za malipo hadi sasa.
Kutokana na madai hayo , Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amemwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Mji kuhakikisha anaisimamia Kampuni ya Nyakiling’ani.
“Mtaro umejengwa mwaka umefika kifusi kile kimekuwa ni mlima na kero kwa wananchi ,wananchi wale wanakwenda kuondoa kifusi hicho sasa ni wito wangu mkateni huyo mkandarasi maana ni ndani ya mkataba wake”Alisema Luhumbi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji mhandisi Modest Apolinary alisema amebaini kuwa kampuni hiyo ina uwezo mdogo wa kutekeleza mradi na kwamba imewekwa kwenye uangalizi baada ya muda wa utekelezaji kuisha.
Kufuatia Malalamiko hayo ya wananchi msemaji wa kampuni hiyo Bw, Raulent Mwita kwa Njia ya simu ameeleza kuwa waliweka kifusi hicho kutokana na ujenzi ambao wanaendelea nao na kuongeza kuwa mvua inayoendelea kunyesha imekuwa ikikwamisha ujenzi.
Post a Comment