GEITA DC YAONGOZA KATIKA MATUMIZI BORA YA VYOO
Msimamizi wa Mradi wa Shirika la maendeleo la nchini Uholanzi (SNV) Bw,Jackson Wandera akizungumza na wadau wa sekta ya afya juu ya mradi ambao ulikuwa umelenga kuhimiza matumizi sahihi ya vyoo. |
Halmashauri ya wilaya ya Geita imeibuka kidedea katika matumizi safi ya vyoo dhidi ya wilaya za Babati, Karatu, Chato na Kwimba zilizoshiriki katika mradi wa Usafi wa mazingira endelevu kwa watu wote uliokuwa ukisimamiwa na Shirika la maendeleo la nchini Uholanzi (SNV).
Hayo yameelezwa na Jackson Wandera wakati wa kikao cha wadau cha kufunga mradi na kuweka mikakati ya kundeleza programu hiyo ulioshirikisha vijiji 72 kwa muda wa miaka minne kuanzia mwaka 2014 hadi machi 31 mwaka huu kwa vijiji ambavyo vilikua havipo katika Mpango wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira(NSC).
“Mwaka 2014 hali ya uchafu wa mazingira ilikua mbaya kutokana na kukosa vyoo safi na bora kwa wakazi wa Geita, ambapo asilimia 24% ya wakazi wa vijiji hivyo 72 walikua wanajisaida vichakani. Asilimia 65% walikua na vyoo vya kawaida, Asilimia 38% walikua na vyoo bora na asilimia 1% tu ndio walikua wananawa mikono yao baada ya kutoka chooni hali iliyopelekea mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu na hii ni sababu kubwa iliyotufanya SNV kuungana nanyi kusaidia jamii ya Geita.” Alisema Wandera
Aidha Wandera ametoa matokeo ya tathimini na kuisifu Halmashauri kupiga hatua na kuondoa tatizo la kujisaidia porini kwa kufikia asilimia 01%ukilinganisha na wakati mradi huu unazinduliwa, Pia wakazi wanaotumia vyoo wamefikia asilimia 95%,wale wenye vyoo bora wamefikia asilimia 87% na wakazi wanaonawa mikono na sabuni baada ya kutoka chooni ni asilimia 04%.
Kwa upande wa mwakilishi kutoka Idara ya elimu Msingi Mwalimu Nassuna Henry alisema tayari elimu ya matumizi safi na bora ya vyoo imefika katika shule zote za msingi 176 na inasisitizwa kutumia vyoo vya safi vinavyosaidia kulinda mazingira na kwa gharama nafuu.
Mradi huo ulishirikisha wilaya za Chato, Geita, Kwimba, Babati na Karatu kwa lengo la kusaidia jamii kuimarisha matumizi bora ya vyoo, Kunawa mikono na sabuni baada ya kutoka chooni na kusisitiza matumizi ya vyoo bora vya safi ambavyo ni vya bei nafuu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Washirika wa maendeleo kutoka shirika la SNV, Watendaji wa Kata, wadau wa SNV vijijini pamoja na waandishi wa habari.
Post a Comment