Simba kuna ‘presha’ kubwa”-Aishi Manula
Golikipa namba moja wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Aishi Manula ameweka wazi tofauti iliyopo kati ya timu mbili ambazo amezitumikia hadi sasa (Azam na Simba) katika ligi kuu Tanzania bara kwa vipindi viwili tofauti.
Manula amabaye amekulia Azam amesema klabu ya Simba ina mashabiki wengi na kuna presha kubwa nyuma yake lakini pia kuna hamasa kubwa ukilinganisha na ilivyo kwa upande wa Azam ambayo ni timu changa inayoendelea kukua siku hadi siku.
“Tofauti iliyopo ni kwamba nipo sehemu ambayo ina mashabiki wengi zaidi, kuna presha kubwa zaidi kutoka kwa watu wanaoipenda hii timu kwa hiyo hamasa ni kubwa zaidi kuliko nilikotoka.”
Manula ndiyo golikipa pekee wa VPL ambaye ameruhusu magoli machache kwenye ligi (amefungwa magoli sita) katika michezo 17 ambayo amesimama kwenye goli la Simba msimu huu. Amesema ubora wake pekeyake hautoshi kumfanya kuwa salama golini bali ushirikiano wa timu nzima ndio unamfanya anonekane imara langoni.
“Ushirikiano wa timu nzima ndio unanifanya niwe bora, hata golikipa uwe unaruka kama nyani huwezi kupambana kuzuia lile goli ambalo ni kubwa kuliko mimi kwa hiyo ni lazima tushirikiane wote kwa pamoja kama timu kuzuia magoli ndiyo maana hadi leo tumekuwa timu iliyoruhusu magoli machache. Ukiangalia tunapocheza mechi zetu mara nyingi mpira unaposimama tunazungumza timu nzima wapi kuna mapungufu na wapi tunafanya vizuri ili kufanya marekebisho tufikie malengo.”
“Kitu kingine ni mazoezi ambayo nafanya pia yanachangia nionekane bora, nipo chini ya kocha mzuri ambaye ana rekodi nzuri kiuchezaji kwa sababu alishaheza timu ya taifa na alicheza nje ya nchi (Msumbiji) kwa hiyo ni kocha ambaye anatufanya kuwa bora.”
Golikipa huyo anatarajia kusimama golini kwenye mchezo wa kimataifa (Caf Confederation Cup) kati ya Simba dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa, mechi hiyo licha kuwa ya kwanza kwa Simba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita lakini kwa Manula ni mwendelezo wa kushiriki mashindano ya Afrika ngazi ya vilabu kwa sababu amefanya hivyo misimu kadhaa akiwa na Azam.
“Huu ni mwendelezo wa kile ambacho nilikuwa nakifanya awali kwa sababu nikiwa Azam kwa misimu mitatu au minne tulikuwa tunashiriki mashindano haya, sasa hivi nimebadili timu kwa hiyo kitu ambacho kipo akilini mwangu ni kuonesha utofauti kama mchezaji nahitaji kutengeneza profile yangu, wakati nikiwa Azam mara nyingi tulikuwa tukiishia hatua za mwanzo nataka kufika hatu nyingine mbele zaidi nikiwa na Simba.”
“Ukiangalia Simba ilishafika hatua kubwa zaidi kwenye mashindano ya kimataifa, sisi pia tunaliangalia hilo kama kipindi cha nyuma wenzetu waliweza kuifikisha mbali klabu yetu tunatakiwa kupigana kuvunja rekodi ambazo tayari zimewekwa na kutengeneza historia mpya kwa kufanya makubwa zaidi kuliko yaliyopo.”
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanja wa Taifa kuipa nguvu timu yao na wenyewe wanaona kama moto basi ndiyo umewaka, tuna kila sababu ya kushinda na nimeshasema tunataka kuweka historia kama wenzetu walivyoweza kuweka historia zao.”
Post a Comment