Marufuku kutangaza dawa za kuongeza makalio
MAMLAKA ya Chakula na Dawa
Tanzania (TFDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini, imepiga marufuku
matangazo ya biashara za vipodozi na dawa za kuongeza maumbile kwenye mitandao
ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, Twitter na blogs.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam,
Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Agnes Kijo alisema matangazo hayo yanatakiwa kukoma
mara moja na wahusika wanastahili kufika katika mamlaka hizo kuomba kibali.
Alisema kumekuwepo na wimbi la watu mbalimbali wanaotangaza
vipodozi kwa lengo la kujichubua na dawa za kuongeza maumbile kwenye mitandao
hiyo ya kijamii wakifanya kinyume na Sheria ya Mamlaka ya Chakula, Dawa na
Vipodozi sura ya 219.
Alisisitiza kuwa matangazo ya vipodozi na dawa hizo
yamekuwa na madai mbalimbali kama vile kuongeza makalio, kuongeza nyonga,
sehemu za siri za mwanaume, kurudisha bikira kwa wanawake na kuondoa mabaka
sugu.
Alisema bidhaa hizo zipo kwenye hali mbalimbali
mathalani vidonge, jeli, losheni, mafuta, krimu na dawa za kunywa. Kijo alisema
baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha umma kuwa bidhaa zao zimethibitishwa na
TFDA kitu ambacho si kweli.
Kwa upande wake, Msaidizi Mkuu kutoka Kitengo cha
Uhalifu wa Makosa ya Kimtandao, Joshua Mwangasa alisema uwepo wa matangazo
katika mitandao ya kijamii ni kinyume na sheria ya mtandao na kwamba inaleta
upotoshaji kwa jamii.
Mwangasa ambaye pia ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi
alisema, “watu ambao wanatumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuweka matangazo
ya dawa na vipodozi vya kuongeza makalio na kukuza maumbile waache mara moja na
wayafute matangazo hayo kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.”
Alisema jeshi hili linaendelea na uchunguzi kuwabaini
wale wote wanaofanya hivyo na kisha watachukuliwa hatua za kisheria.
Post a Comment