Header Ads

Rais Magufuli Aipa Siku 5 Wizara ya Kilimo

Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha mbolea inafikishwa katika mikoa yote ya uzalishaji wa chakula ukiwemo Mkoa wa Rukwa ifikapo Ijumaa Januari 12, 2018.

Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu wakati akimwapisha Mhe. Dotto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri wa Madini Ikulu jijini Dar es Salaam. 

Amemuelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatilia jambo hilo na amebainisha kuwa endapo mbolea haitafikishwa katika maeneo hayo ifikapo Ijumaa wahusika waachie ngazi.

“Wakulima wanataka mbolea na muda ni huu, inasikitisha sana, fedha kwenye bajeti zimetengwa lakini mpaka leo mbolea haijawafikia wakulima, sasa mkoa kama Rukwa ndio tunaoutegemea kwa chakula, waziri yupo na watendaji wake wapo lakini mpaka leo mbolea haijapelekwa, wakulima watazalishaje chakula?

Rais Magufuli amewataka watendaji wote wa Serikali kutekeleza majukumu yao ipasavyo na ameonya kuwa hatosita kumfukuza kazi mtendaji yeyote atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya Watanzania.

“Nataka kila mmoja afanye kazi, Watanzania wanataka maendeleo, hakuna muda wa kubembelezana, kila mmoja afanyie kazi mambo yanayomhusu asisubiri kuambiwa, kule bandarini niliunda timu za kuchunguza madudu yaliyopo huko naambiwa kuna makontena 178 ya makinikia hayana mwenyewe, mengine yapo Ubungo, mengine bandari” ameongeza  Rais Magufuli.

No comments