Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo Akizungumza na waandishi wa Habari juu ya tukio la kuandamana wa madiwani wa Halmashauri mbili za Mji na Wilaya.
Jeshi la polisi Mkoani Geita linamshikilia Mbunge wa Jimbo la Geita Joseph Kasheku Msukuma kutokana na tukio la maandamano ambayo yalifanyika siku ya Alhamisi wiki hii yaliyopelekea uharibifu wa miundombinu ya maji kwenye mgodi wa GGM.
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoani Geita,Mponjoli Mwabulambo amezungumza na BAHEBE STAR ambapo amesema kuwa wanawashikilia madiwani sita pamoja na mbunge huyo kwa ajili ya kufanya nao mahojiano ambayo yatabaini ni akina nani ambao wamehusika na tukio hilo la kuandamana kinyume na sheria.
Amesema kuwa Mbunge huyo wamemkamata majira ya mchana siku ya jana mjini Geita na kwamba wanaendelea na mahojiano ambayo yatasaidia kuwabaini wale ambao walihusika na tukio.
Kamanda Mponjoli amesema jeshi lake linaendelea na msako wa kuwabaini,kuwakamata na kuwachukulia hatua wale wahusika wa tukio hilo na kwamba sheria ya makosa ya jinai haina kikomo na kwamba mtu akifanya kosa leo na akakwepa ataendelea kutafutwa,na hana namna ya kuukwepa Mkono wa sheria.
Mapema wiki hii ,jeshi hilo lililazimika kutumia nguvu
kutawanya maandamano ya madiwani pamoja na wananchi
walioweka vizuizi katika barabara inayoingia mgodini
wakishinikiza kulipwa ushuru wa huduma kiasi cha dola za
kimarekani milioni 12.65 ambazo ni sawa na zaidi ya
shilingi Bilioni 26.
|
Post a Comment