Header Ads

Mbowe Alaani Wabunge wa CHADEMA Kukamatwa......Aiomba Mahakama Itende Haki

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mh. Freeman Mbowe amelaani kitendo cha wabunge 8 wa upinzani kukamatwa na jeshi la polisi kwa madai yakutaka kumpiga mbunge wa CCM Juliana Shonza, na kusema hawajapeleka mabondia bungeni.

Freeman Mbowe aliyasema hayo  jana mjini Dodoma baada ya kutoka mahakamani na kudai kuwa wao wanaamini kuwa mahakama itatenda haki kwa wabunge hao.

"Kama ambavyo mnajua kwa masaa zaidi ya 48 wabunge wa CHADEMA wameshinda polisi, jana siku nzima wameshinda polisi na leo wameshinda polisi mpaka mchana huu.

"Kwa maana hiyo wawakilishi hawa wa wananchi wameshindwa kuwajibika kwa ajili ya wananchi kwa makosa ambayo kimsingi kabisa hayakutakiwa kupewa uzito huu yanaopewa.

"Inasemakana kuwa wabunge hawa walimfanyia fujo Mbunge wa viti maalum (CCM) Juliana Shonza, jambo hili linafedhehesha sana, sisi tuna wabunge ambao wanajiheshimu na kuheshimu sheria za nchi, hatukupeleka wapiganaji bungeni bali tumepeleka viongozi wa kutunga sheria" alisisitiza Freeman Mbowe

Mbali na hilo Mbowe anasema kitendo cha Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai kulivalia njuga suala hilo ni jambo ambalo yeye limemsikitisha.

"Kitendo cha kuwapeleka polisi na kuwashtaki wabunge wetu na Spika wa Bunge kushadadia jambo hili limenisikitisha sana

" Spika kusema ametoa ruhusa wahukumiwe kwa kesi za jinai ni mwendelezo wa kutaka kutunyamazisha, ila hatutayumba na tunaamini kuwa jopo la majaji litatenda haki katika jambo hili, maana hakuna mbunge yoyote wa CHADEMA wala UKAWA ambaye amemshambulia mbunge yoyote yule bungeni" alisisitiza Mbowe.

Katika watuhumiwa wote nane, mtuhumiwa mmoja ambaye ni Mbunge wa jimbo la Ubungo, Mbunge Saed Kubenea jana  alipandishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa moja la shambulio la kawaida hivyo alidhaminiwa na shauri hilo upelelezi wake bado haujakamilika hivyo kesi itatajwa tena tarehe 26, Julai 2017 Dodoma.

No comments