Header Ads

Mvua yatesa familia Pemba

MVUA za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali Zanzibar zimeleta athari kubwa kwa familia kadhaa kukosa makazi kisiwani Pemba huku ghala la karafuu likijaa maji na mazao kuharibika.

Wakati hayo yakitokea wananchi wamelazimika kuhama makazi baada ya nyumba zao kuingia maji.

Kwa upande wa kisiwani Pemba familia zaidi ya 80 zimekosa makazi na ghala la kuhifadhia karafuu lililopo Mkoani limebomoka na kusababisha karafuu zilizokuwamo humo kuharibika baada ya kuingia maji.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwajuma Abdallah Majid,alisema kuwa madaraja yaliyobomoka kutokana na mvua hizo ni ya Kiwani,Pujini na Chonga.

Alizitaka familia za wananchi walioathirika na mvua hizo kuwa na moyo wa subra huku serikali inaendelea kufanya tathmini ili kujua hasara za gharama za nyumbani na miundombinu iliyoathirika.

Hata hivyo, alisema wananchi waliokosa makazi kutokana na nyumba zao kuathiriwa wamehifadhiwa na ndugu na jamaa.

Aidha zimeathiri miundombinu mbalimbali ya barabara na madaraja kubomoka hali ambayo imesababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na madereva wa vyombo vya usafiri barabarani.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti walioathirika na mafuriko wanasema kuwa mvua hizo zimesababisha baadhi ya huduma kusimama kwa muda mrefu ikiwamo usafiri wa daladala na biashara za maduka na sokoni.

Walisema kuwa baadhi ya barabara hasa Kisiwani Pemba zimeathirika zaidi na madaraja matatu yamebomoka pamoja na barabarba ya Mwanakwerekwe na Fuoni , Kibonde Mzungu, Unguja kwa vile maji yametuama kwa wingi jambo ambalo lilisababisha madereva wa gari za abiria kusitisha shughuli za usafirishaji

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed, alisema athari za mvua hizo tayari zimeanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo yenye kiwango kikubwa cha mvua hasa kisiwani Pemba.

Waziri Aboud , aliiagiza Mamlaka ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, kuratibu matukio yote yanayosababishwa na athari za mvua hizo ili serikali ianze kushughulikia.

No comments