Vita dhidi ya dawa za kulevya: Masogange adaiwa kukamatwa na polisi
Taarifa zinadai kuwa mrembo Agnes ‘Masogange’ Gerald amekamatwa na polisi usiku wa kumkia leo, ikiwa ni sehemu ya msako wa watu wanaohusishwa na biashara ya dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Jamii Forums, Masogange anashikiliwa kwenye kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam.
Mrembo huyo anakuwa staa mpya kuingizwa kwenye orodha ya mastaa wengine waliohusiswa na sakata hilo.
Kwenye mazungumzo yaliyovuja hivi karibuni na kusambaa mtandaoni, Wema Sepetu aliyekuwa ameshikiliwa pia kituoni hapo kwa sakata kama hilo, alisikika akimtaja Masogange kuwa mmoja wa mastaa wanaoshukiwa kujihusisha kwenye biashara hiyo.
Hiyo sio mara ya kwanza kwa Masogange kushikiliwa na polisi kwa tuhuma hizo. August 2014, Kikosi Kazi cha Polisi cha Kuzuia Dawa za Kulevya nchini kilimhoji kwa zaidi ya saa 10 mrembo huyo kuhusiana na tuhuma za kukamatwa na dawa aina ya crystal methamphetamine huko Afrika Kusini, Julai mwaka 2014.
Masogange alitawala vyombo mbalimbali vya habari nchini mwaka 2014 baada ya kukamatwa Afrika Kusini akiwa na nduguye Melisa Edward wakiwa na ‘mzigo’ wa dawa hizo zenye thamani zaidi ya Sh6.8 bilioni.
Wasichana hao walinaswa baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakitokea Tanzania.
Katika mahojiano hayo, Masogange alidai kuwa alipewa dawa hizo na mtu ambaye hamfahamu kwa jina lakini anaikumbuka sura yake.
Post a Comment