Header Ads

KIHESHIMU KIDOGO ULICHONACHO.

Kama upo kwenye safari ya mafanikio jifunze sana kutokuwa na dharau na kile kidogo ulichonacho. Kama una kitu ambacho ni kidogo iwe pesa au uwezo fulani au kitu chochote ambacho unaona ni kidogo kithamini sana kitu hicho.

Kitu nilichojifunza katika safari ya kutafuta mafanikio ni kwamba, mafanikio mara nyingi huweza kuanza kidogo kidogo sana mithili ya mbegu ya haladari. Kazi ya kukuza au kupapalia kile kidogo ulichopewa ili kiwe kikubwa sasa hapo ndiyo inakuwa  kazi yako.

Kwa mfano, kama ni pesa huwezi kuanza na kuwa na pesa nyingi mara moja, katika maisha yako unaweza ukaanza na pesa kidogo tu, lakini hizo pesa kidogo ukazifanya kama mbegu na kuwekeza huku na huko na baadae kuwa pesa nyingi.

Kama ni gari, nyumba, mtaji au maarifa fulani vyote hivyo huwa vinaanza kidogo kidogo na baadae kuwa vitu vikubwa vya kushangaza. Chochote ambacho unacho hata kama ni kidogo acha kukidharau hata kidogo zaidi kiheshimu.

Mafanikio yote makubwa yaliyopo duniani huwa yanaanza kwa kidogo sana. Hebu angalia miti mikubwa kama mibuyu ambayo inaishi zaidi ya miaka hata 500 nayo ilianza kama mchicha tena kukua kwake kukiwa kwa tabu.

Tambua Hakuna mafanikio ambayo yanaanza juu kabisa. Asili ya mafanikio yote makubwa yanaanza kwa kuanzia chini. Hizo ndizo hatua za mafanikio. Wakati wote mafanikio yapo kama hatua za mtoto mdogo ni lazima atambae kwanza kabla ya kutembea, na mafanikio yapo vivyo hivyo.

Kwa hiyo kwa kulijua hilo chochote ulichonacho hata kama ni kidogo vipi, mshukuru MUNGU kwa hicho na kisha kifanye kiwe mbegu kwako ya kukusaidia kufanikiwa. Acha kuwa na dharau na kidogo ulichonacho na kama ukiwa na dharau hutafika popote.

Kama una pesa kidogo zitunze. Kama unafanya kazi unayolipwa mshara mdogo iheshimu kwanza kazi hiyo, na halafu ile pesa kidogo unayoipata ifanye kuwa kama mbegu ya kukusaidia kufanikiwa katika maisha yako kwa kuiwekeza.

Hapo ulipo hata kidogo acha kuogopa kwa jinsi unavyoteseka na kusota kwa sababu ya kukosa pesa au maisha magumu, ninachotaka kukwambia huo ni mwazo tu wa mafanikio yako. Usikate tamaa endelea kupambana, Mungu yupo pamoja nawe.

Hakuna kitu ambacho hakibadiliki hata maisha yako yanakwenda kubadilika ikiwa hutakubali kushindwa na ukawa mtu wa kuchukua hatua. Siku zote kumbuka kuthamini kile kidogo ulichonacho.
Soma; Mambo Ya Kufanya Kila Siku, Ili Kujenga Mafanikio Makubwa.

Kama unakumbuka katika maandiko matakatifu wakati wana wa Israel wakiwa wamekosa tumaini na kuamini ni lazima wafie katika bahari ya shamu, lakini Mungu aliwaokoa kupitia fimbo aliyokuwa nayo mtumishi wake Mussa.

Hata wewe hapo ulipo kipo kitu  ambacho unacho hutakiwi kukidharau. Kama Mussa angeizarau fimbo yake na kusema kwamba isingeweza kufanya kitu basi wana wa Israel wangefia wote katika bahari ya shamu.

Kwa chochote ulichonacho, chukua hatua. Kiheshimu hicho ulichonacho na kifanyie kazi. Kama unaona unapata pesa kidogo sana, ziweke pesa hizo, acha kuzitumia hovyo na kusema haziwezi kunisaidia kitu.

Hivyo, ili kufanikiwa ni lazima utambue mafanikio yako huwa yanaanza kwa kidogo sana. Jukumu la kuyakuza na kuyafanya yawe makubwa lipo mikononi mwako. Kama ni mbegu ya mafanikio tayari unayo, acha kulaumu chochote zaidi, heshimu kidogo ulichonacho na utafanikiwa.

No comments