Header Ads

Jela miaka 30 kwa kumbaka bintiye

MAHAKAMA ya Wilaya ya Lindi, imemhukumu mkazi wa Kata ya Wailes, Halmashauri ya manispaa hiyo, Issa Salum Nambaruka (60), kutumikia kifungo cha miaka (30) jela baada ya kupatikana na kosa la kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka (14) (jina limehifadhiwa).

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Erasto Phiri, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka akiwamo na mlalamikaji mwenyewe.

Kabla ya mshtakiwa kupewa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Phiri, alimpa nafasi ya kujitetea ambapo aliomba apunguziwe adhabu kwa madai kuwa hilo ni kosa lake la kwanza na ana familia inayomtegemea wakiwamo wazazi, mke na watoto.

Hata hivyo, Mwanasheria wa Serikali, Abddulrahman Mohamed, aliiomba mahakama impe adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wazazi wengine walio na tabia ya kuwabaka watoto wao.

“Mheshimiwa Hakimu, kupitia Mahakama yako tukufu, naomba umpatie mshtakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wazazi wenye tabia ya aina hiyo,” alisisitiza Mohamed.

Akitoa hukumu katika kesi hiyo, Hakimu Phiri alisema:

"Nimesikiliza na kuzingatia maombi ya pande zote mbili, lakini kutokana na sheria kunifunga mikono, nashindwa kwenda kinyume, hivyo namhukumu mshtakiwa Issa Salum Nambaruka, kifungo cha miaka 30 jela."

“Nimeyasikia maombi yenu, lakini kutokana na kushamiri kwa vitendo hivi, upande mwingine hauwezi kumpatia unafuu, kutokana na sheria kunifunga mikono, hivyo mshtakiwa unalazimika kwenda gerezani miaka 30,” alisisitiza hakimu.

Awali, ilidaiwa na Mwanasheria wa Serikali, Mohamed kuwa Novemba na Desemba, mwaka 2016, nyumbani kwake Kata ya Wailes Manispaa ya Lindi, mshtakiwa bila ya huruma, alimbaka mtoto wake wa kumzaa ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita na kumsababishia maumivu sehemu zake za siri.

Katika kesi hiyo, mashahidi wanne akiwamo mlalamikaji, mama wa kambo wa mlalamikaji, mwenyekiti wa serikali ya mtaa na daktari aliyemfanyia uchunguzi mlalamikaji, walitoa ushahidi wao.

No comments