Wahanga 15 wakiwemo watanzania 14 na raia mmoja wa kichina walionusurika na kifo baada ya kuokolewa kutoka chini ya ardhi kwenye mgodi wa dhahabu wa RZ union ulioko kijiji cha Mawemeru kata ya Nyarugusu mkoani Geita baada ya kukaa siku 3 bila chakula wala huduma yoyote wameruhusiwa kutoka Hospital ya mkoa wa Geita walikopelekwa kupata matibabu.
Akiwaaga baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali Mkuu wa Mkoa wa Geita,Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga,amewaomba kurudi na kuendelea kujituma katika shughuli ambazo wanafanya ili kuendelea na ujenzi wa Taifa.
“Mko imara sasa mrudi mkaendelee tena na ujenzi wa Taifa letu shughuli hizi ndio zitawasaidia kupata kipato tumefarijka sana miongoni mwenu hayupo hata mmoja aliyeteteleka”Alisema Kyunga.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Geita,Mwl Herman Kapufi,amesema kuwa wamekubaliana na mgodi huo wafanyakazi wote katika mgodi huo kupatiwa mkataba ambao utawasaidia wafanyakazi, na pia amewaomba kuwa na mahusiano mazuri baina yao (wafanyakazi) na Waajiri ambao ni Raia wa china na pia amewasisitiza kumrudia Mungu kwani amewanusuru na kifo.
Aidha kwa upande wake Mwanasheria wa mgodi huo,Francis Kiganga pamoja na kuwashukuru watu waliojitolea kufanya shughuli za uokoaji pia amemhakikishia mkuu wa wilaya kuongeza mkataba wa kazi badala ya miezi mitatu atawapa wa mwaka mzima.
Akiwaruhusu wahanga hao, mganga mfawidhi wa Hospital ya mkoa wa Geita Dk. Brian Mawalla amesema wamefikia uamuzi wa kuwaruhusu baada ya kujiridhisha na maendeleo mazuri ya afya zao.
Wahanga hao Wameokolewa January 29 mwaka huu kwa msaada kutoka makampuni ya Busolwa Mining,Nyarugusu,GGM na ACACIA wamefanikiwa kuwaokoa watu hao waliofukiwa na udongo wa kifusi cha mgodi huo Januari 26 mwaka huu.
Post a Comment