Rais Dkt.magufuli afanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Chato
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 9 Januari, 2017 amefanya ziara ya
kushtukiza katika Shule ya Msingi Chato,ambapo ndipo aliposoma kuanzia darasa
la kwanza hadi la saba na kuzungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Rais Dkt Magufuli ameahidi kujenga
madarasa matatu na ofisi moja ya walimu katika Shule hiyo kufuatia ombi la
Walimu kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa
ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo.
Aidha Dkt.Magufuli amewaasa wanafunzi
kutilia mkazo masomo ili waweze kufaulu na kuwataka walimu
kuhakikisha wanatumia vyema fedha zinazotolewa na Serikali kila mwezi katika
kutoa elimu bila malipo na pasiwe na wanafunzi hewa kama ilivyo kwa baadhi
ya shule ambazo zimegundulika kuwa na wanafunzi hewa katika uhakiki uliofanywa
na serikali.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule
ya Msingi Chato, Bwana Mwita Chacha amemshukuru Rais Dkt.Magufuli kwa
msaada aliowapatia katika kukabiliana na uhaba wa madarasa uliokuwa unaikumba
shule hiyo, pia kuitembelea Shule yao jambo ambalo
limewatia moyo walimu na wanafunzi shuleni hapo.
Rais Magufuli pia ametembelea eneo la
Stand ya zamani na kuzungumza na baadhi ya wananchi waliokuwepo eneo hilo na
kutoa msaada kwa kikundi cha wasafisha viatu ili kuongeza mtaji
wa biashara yao.
Jaffar
Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita.
9 Januari, 2017
Post a Comment