"Ngoma ya Darassa haina ujumbe"
Darassa
Msanii mkongwe wa bongo fleva, Prince Dully Sykes amesema wabongo wengi hawapendi nyimbo zenye ujumbe wa kuhamasisha maendeleo, na ndiyo maana ngoma nyingi zisizokuwa na ujumbe wa aina hiyo ikiwemo ya 'Muziki' ya Darassa, huwa zina hit zaidi.
Dully alizungumza hayo hivi karibuni akiwa kwenye kipindi cha Planet Bongo cha EA Radio, alipokuwa akizungumzia mikakati yake kwa mwaka 2017 na kutakiwa kuelezea maana ya ngoma yake ya 'Inde' ambayo ilikuwa 'hit' mwaka 2016.
Alisema wimbo wa Darassa hauna ujumbe wowote wa kuhamasisha maendeleo isipokuwa umejaa majigambo na kujisifia, na kwamba nyimbo za aina hiyo ndizo hupendwa na watanzania huku akisema kuwa endapo Darassa angeimba maendeleo, wimbo wake usingependwa.
"Kwani wimbo wa darassa una ujumbe gani? siyo simba, siyo chui, hiyo si ni kujisifia tu, wabongo ukiwaimbia eti sijui twende tukalime, tufanye kazi maendeleo na vitu kama hivyo hawavipendi" Alisema Dully.
Alisema kwa kutambua hivyo, ndiyo maana na yeye hawezi kutunga nyimbo zenye ujumbe wa maendeleo na ataendelea na ngoma kama ilivyo 'inde' na nyingine ambazo zimetikisa anga la bongo fleva
Dully
Hata hivyo, Dully alimpongeza Darassa kwa kazi nzuri na kwa kulishika game la bongo kwa kipindi hiki, na kukiri kuwa kazi yake ni nzuri huku akikataa kuwa ngoma ya Darassa haijamfunika kwa kuwa ngoma yake ya 'inde' ilikuwa hit kabla ya 'Muziki' ya Darassa.Kuhusu ujumbe uliomo kwenye ngoma ya 'inde' Dully alisema ngoma hiyo aliitengeneza kwa ajili ya kucheza kuburudisha zaidi maana hicho ndicho watanzania wanachokipenda, huku akikanusha kuimba matusi na kusema "Sijaimba matusi, ni jinsi wewe utakavyoutafsiri na kuuelewa, tuliza akili yako utajua nimeimba nini, vitu vingine havisemwi hadharani"
Kuhusu mikakati yake ya mwaka 2017, Dully amesema muda si mrefu atatoa ngoma nyingine ambayo anaamini itakuwa ni kali zaidi ya 'inde' na kuwataka mashabiki wake wakae mkao wa kula.
Post a Comment