Header Ads

KUFA NA MIAKA 35 NA KUZIKWA NA MIAKA 65.

Kuna utaratibu fulani wa maisha ambao watu wengi sana kwenye jamii wanajikuta wanaufuata bila ya wao wenyewe kujua. Na kwakuwa watu wengi hawana mipango kwenye maisha yao wanajikuta wanafata kile ambacho kila mtu kwenye jamii anafanya.
  Kama una miaka zaidi ya thelathini na tano au kama umeshakaa kwenye ajira zaidi ya miaka mitano kuna uwezekano mkubwa umeshakufa na unasubiri kuzikwa. Kama bado hujafikia umri huo na bado hujakaa kwenye ajira kwa kipindi hiko bado haupo salama sana kwa sababu kama usipokuwa makini unaelekea kwenye kifo hicho cha ajabu.
  Kwa umri wowote ulionao, iwe umeshakufa ama unaelekea kufa(kifo ambacho nitakielezea hivi punde) ni vyema ukasoma hapa na kubadili maisha yako ili uanze kuishi tena.
35
  Hebu tuangalie maisha yako na ya wengi kwa ujumla yanakwendaje. Ulizaliwa, ukakua kama mtoto mwenye furaha, kila ulipoulizwa ukikua unataka kufanya nini ulijibu kwa kujiamini na bila shaka yoyote. Ukaenda shule ya msingi, baada ya miaka saba ukamaliza, mpaka wakati huu mambo mengi uliyokuwa unawaza ukiwa mtoto unaanza kuona hayawezekani na kuona utoto ndio ulikuwa unakudanganya.
  Ukaenda sekondari ama mafunzo mengine nako kwa zaidi ya miaka minne ukaendelea kupotea kwenye ndoto zako na kusisitiziwa kwamba kusoma na kufaulu ndio kupata kazi na maisha mazuri.
  Baada ya sekondari ukaingia chuoni(wengine vyuo vikuu, wengine vyuo vya ufundi), kwenda kusomea ujuzi, inawezekana ni moja ya machaguo yako ama ndicho kilichopatikana kutokana na ufaulu wako. Huko chuoni nako ukazidi kuziteketeza ndoto zako na kujifunza kuwa mfanyakazi mzuri, jinsi ya kuomba kazi na ukatumia muda wako mzuri kujifunza mbinu mbalimbali za kushinda usahili wa kazi.
  Baada ya kuhitimu mafunzo ya chuoni ukarudi mtaani, ukasota kidogo au sana au ukapata kazi. Ukaanza kazi ukiwa na matumaini makubwa na mipango mingi ya kutokaa sana kwenye ajira. Hivyo ukapanga kufanya kazi kwa kipindi fulani ila baadae uanzishe kazi yako na wewe uajiri watu wengine.
  Kote huko mambo yanaweza kuwa yamekwenda vizuri ama ulikutana na vikwazo vya hapa na pale ila ukavivuka. Tatizo kubwa linaanza miaka mitano baada ya kuanza ajira. Mpaka kumaliza chuo unakuwa na miaka 25 na mpaka kupata na kukaa kwenye ajira ni karibu miaka 35.
  Watu wengi ambao wameshakaa kwenye ajira zaidi ya miaka mitano inakuwa ngumu sana kwao kuondoka kwenye ajira. Na kibaya zaidi ndani ya miaka hiyo wengi ndoto zao zinakuwa zimezima kabisa, mipango mikubwa waliyoweka wakati wanaanza ajira wanaona haiwezekani tena.
  Wengi wanajikuta na matatizo mengi ambayo yanawafanya waamini bila kazi hiyo maisha hayawezekani. Majukumu ya familia yanakuwa mzigo mkubwa, gharama za maisha nazo zinafanya kipato kisitoshe. Kwa wakati huu unakuwa unaishi kwa kuhesabu mwisho wa mwezi.
  Mbaya zaidi unajikuta umeingia kwenye madeni yanayozidi kipato chako hivyo kila siku ni matatizo. Unajikuta muda mwingi unakaa kufikiria matatizo hayo na hivyo kusahau kabisa ndoto kubwa na nzuri ulizowahi kuziwaza kwenye maisha yako. Huu ndio wakati ambao UMEKUFA ILA BADO UNAENDELEA KUTEMBEA.
  Umekufa kwa sababu hakuna kitu kipya kinachoendelea kwenye maisha yako. Unaamka asubuhi, unakwenda kazini, unarudi nyumbani kesho hivyo hivyo. Muda mwingi unautumia kuwaza matatizo unayokutana nayo kila siku. Huna tena muda wa kuwaza ndoto kubwa ulizokuwa nazo, huamini kama unaweza kuishi maisha nje ya ajira. Na huenda matatizo ya mahusiano na ya kifamilia yameshakuvuruga kabisa. Huna mpango mpya na maisha yako zaidi ya kufanya kile ulichofanya jana, na kurudia tena kesho. Hapo unakuwa umekufa na unasuburi kuzikwa.
  Baada ya kukaa kwenye ajira kwa muda mrefu unafikia wakati wa kustaafu. Hapa unapata faraja kidogo kwamba ukistaafu utalipwa mafao yako na hivyo utaweza kujikwamua kimaisha. Ni mpango mzuri ila nikutahadharishe kitu kimoja kama bado huna mpango na maisha yako mambo yataendelea kuwa hivyo hivyo.
  Tafiti zinaonesha watu wengi wanakufa ndani ya miaka mitano baada ya kustaafu. Zipo sababu nyingi za vifo hivyo na baadhi ni mabadiliko ya maisha na kukata tamaa kutokana na kukosa chanzo cha mapato na kutumia vibaya fedha za mafao. Hivyo kama umestaafu na miaka 60, miaka mitano baadae kuna uwezekano mkubwa ukapelekwa kaburini.
  Hii ndio dhana kubwa ya kufa ukiwa na miaka 35 na kuzikwa ukiwa na miaka 65. Kwa sababu baada ya kukolea kwenye kazi(miaka 35) hakuna kipya kinachoendelea kwenye maisha yako na baada ya kustaafu miaka mitano baadae unapelekwa kaburini(miaka 65).
  Siandiki haya kukutisha ama kukukatisha tamaa. Lengo kubwa hapa ni TUJIELEWE NA TUJUE THAMANI YA MAISHA YETU. Kama bado hujafikia kwenye hatua hizo jipange kutoingia na kama umeshaingia kwenye hatua hizo fanya maamuzi mara moja kujikomboa kutoka huko.
  Utajipangaje kutoingia ama utajipangaje kutoka kwenye hali hiyo?
  Kama mpaka sasa bado hujajua ni jinsi gani unavyoweza kuchukua hatua dhidi ya maisha yako soma makala nyingi zilizomo kwenye blog hii 
  Tumeona wazazi wetu, ndugu jamaa na marafiki wanavyoishi maisha magumu sana kwa staili hiyo ya maisha. Tujitahidi kutoingia kwenye mtego huo na kama umeshaingia fanya maamuzi ya kuondoka haraka iwezekanavyo.

No comments