Header Ads

Kim Kardashian avamiwa na watu wenye silaha

Nyota wa televisheni nchini Marekani Kim Kardashian .

Nyota wa televisheni nchini Marekani Kim Kardashian ameshambuliwa na kuzuiliwa na watu waliokuwa na silaha katika hoteli moja mjini Paris, taarifa zinasema

Msemaji wake anasema nyota huyo wa uigizaji wa vipindi vya maisha ya uhalisia alizuiliwa na watu waliokuwa wamejifanya maafisa wa polisi na ambao walikuwa wamejifunika nyuso zao.

"Ameshtushwa sana na tukio hilo lakini hajaumizwa," msemaji wake amesema.

Mumewe Kanye West amekatisha ghafla tamasha ambalo amekuwa akishiriki mjini New York kutokana na tukio hilo.

Kanye West alikuwa akitumbuiza katika tamasha ya Meadows Music and Arts Festival na amesitisha ghafla utumbuizaji na kuwaambia mashabiki kwamba alikuwa na "dharura ya kinyumbani".

"Nawaomba radhi, nina dharura ya kinyumbani na inanibidi kukomea hapa kwa sasa," West aliwaambia mashabiki.

Kardashian West alikuwa ameenda Paris, pamoja na mamake Kris Jenner na dadake Kendall Jenner, kuhudhuria maonyesho ya mitindo.

Alihudhuria maonyesho ya Givenchy Jumapili jioni.

Wiki iliyopita, alikabiliwa na Vitalii Sediuk, mtu mwenye mazoea ya kukabili watu mashuhuri alipokuwa akijaribu kuingia kwenye mgahawa.

Paris ni mji unaopendwa sana na Kardashian na mumewe.

Wawili hao walikaa mjini humo wikendi iliyotangulia kabla yao kufunga ndoa mjini Florence Mei 2014.

Haijabainika iwapo watoto wa wawili hao, North mwenye umri wa miaka 3 na Saint mwenye umri wa miezi 10, walikuwa kwenye hoteli hiyo na Kardashian.

No comments