Header Ads

BURUNDI YAAMUA KUJIONDOA ICC.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza.
 Serikali ya Burundi ambayo imeamua kuchukua uamuzi wa kujiondoa kuwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Uamuzi huu unakuja baada ya wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa kutoa orodha ya viongozi 12 serikalini ambao wanatuhumiwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu nchini Burundi.
Inaelezwa kuwa watu hao karibu wote ni washirika wa karibu wa Rais Pierre Nkurunziza, na na uamuzi wa kujiondoa kuwa mwanacahama wa ICC ulichukuliwa katika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Alhamisi wiki hii.
Uamuzi wa Burundi umekuja wakati huu ambapo baadhi ya nchi za Afrika zinazishawishi nchi nyingine kujitoa kwenye mahakama hiyo kwa sababu ya kile wanachodai kuwa mahakama hiyo inawalenga viongozi wa Afrika peke yake. Msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba, amethibitisha kutoka mjini Bujumbura kwamba uamuzi huo umechukuliwa na kwamba kinachosalia ni kupitishwa na Bunge pamoja na baraza la seneti.
Itafahamika kwamba maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi, polisi na baadhi ya maafisa serikalini nchini Burundi wanatuhumiwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu kuhusika na vitendo viovu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mauaji na mateso dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu, wanasiasa na wafuasi wa upinzani.
Wakati huo huo Mwendesha mashataka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, amesema kuwa, itakuwa siku ya huzuni kubwa ikiwa nchi za Afrika zitaamua kujitoa kwenye mkataba Roma unaotambua mahakama hiyo.
Fatou Bensouda ametoa wito kwa wakuu wa nchi za Afrika kuachana na mpango wao wa kujiondoa kwenye mahakama ya ICC, akisema kufanya hivyo kutawanyima wananchi wengi wa Afrika haki na wahalifu kuendelea kulindwa.

No comments