Header Ads

HEKIMA INAHITAJIKA KATIKA HILI.


Tarehe 27 Julai mwaka huu chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kilitangaza kuwa kitafanya maandamano nchi nzima,ambapo Oparesheni hiyo ilipewa jina la UMOJA WA KUPAMBANA NA UDIKTETA TANZANIA (UKUTA) huku madai makuu yakiwa ni kukandamizwa kwa DEMOKRASIA hapa nchini na nchi kuongozwa kwa kauli za mtu mmoja (RAIS).
Maandamano hayo kwa kauli ya CHADEMA yatafanyika kuanzia tarehe moja Septemba.!
Baada ya kauli hiyo ya CHADEMA zilifuata kauli za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli,alizotamka kwa nyakati tofauti wakati akiwa kwenye ziara yake katika mikoa ya Singida,Shinyanga, Mwanza,Tabora na Geita.Miongoni mwa kauli hizo ni pamoja na hii aliyoitoa akiwa Singida;

“Sitaki nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia kikamilifu bila huruma, na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala sitajaribiwa.

“Wananchi hawa wana shida, na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate dawa, nataka hao wanaotetea maandamano watangulie wao halafu wataona cha mtemakuni" Alisema Rais Magufuli.

Wengi walitoa mitazamo yao tofauti kufuatia matamko hayo.Na hivi karibuni kumekuwa na utaratibu wa jeshi la polisi kufanya mazoezi katika maeneo ya wazi wananchi wakishuhudia,jambo hili limezua maswali miongoni mwa wengi licha ya polisi kuwatoa hofu wananchi kuwa hali hiyo ni ya kawaida kwa jeshi hilo ili kuweka sawa miili yao.

Binafsi namuunga mkono Mh.Rais kwa jitihada zake za kuhakikisha Tanzania inafika mahali pa neema chini ya kauli mbiu ya "HAPA KAZI TU" Lakini pia nipende kuikumbusha serikali ya awamu ya tano kuwa Tanzania ni nchi ya Kidemokrasia yenye vyama vingi.
Hivyo badala ya kutumia nguvu nyingi kiasi hicho ni vyema sasa ikatumika Hekima na Busara! Serikali ikae na wapinzani ili kuona ni kwa namna gani wataleta ufumbuzi kwa yale yanayoonekana kwenda tofauti kwani mwisho wa siku FAHARI WAWILI WANAPOPIGANA NYASI NDIO HUUMIA.
Jambo lililonishtua zaidi ni pale ambapo umoja wa vijana wa Chama cha mapinduzi UVCCM kutangaza kuwa na wao watakuwa na maandamano ya amani nchi nzima siku moja kabla ya Chadema kufanya hivyo,huku wao wakieleza kuwa wanafanya hivyo kwa lengo la kwenda kuwaeleza wananchi kazi zinazofanywa na Rais Magufuli sambamba na kuunga mkono juhudi zote za serikali ya awamu ya Tano.

Swali langu hapa ni Je,wananchi hawaoni hadi wakaelezwe? Ni sawa kuunga mkono kwa maandamano badala ya kufanya kazi? Je,imeshindikana kabisa kutafuta au kudai demokrasia kwa njia zingine hadi maandamano?
Ninachokiona mimi ni machafuko kwani kama Chadema watashikilia msimamo wao na UVCCM wakaendelea na uamzi wao kama walivyosema wao kuwa "Tumeomba polisi watulinde na kama hawatatulinda tutajilinda wenyewe!!" Huku polisi nao wakipiga zoezi sipati picha nini kitatokea.

Ni maombi yangu kwa Mh.Rais Magufuli ajaribu kukaa na viongozi hawa wa Upinzani ili kutafuta suluhu na sio kuishia kutoa matamko kwenye majukwaa! Tanzania ni nchi ya amani,hivyo tusingependa kuona sifa hiyo ikipotea na watu kuanza kukimbia hovyo,"LINALOWEZEKANA LEO LISINGOJE KESHO", na huu tayari ni ufa tena "USIPOZIBA UFA UTAJENGA UKUTA" Niombe Serikali pamoja na vyama vya siasa hebu kaeni na kuziba huu UFA uliopo na tusisubiri KUJENGA UKUTA kisha kuhangaika KUUVUNJA.





No comments