Sheikh Ponda Issa Ponda Ponda afurahia Magufuli kurejesha mali za Waislamu
Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda amempongeza Rais John Magufuli kutokana na ahadi yake ya kurejesha mali za Waislamu.
Lakini Sheikh Ponda hajakubaliana na kitendo cha Rais kutoa fedha taslimu kwa ajili ya kuchangia safari za Hija, akisema mkuu huyo wa nchi angezungumza na wahusika ili kujua matatizo ambayo fedha hizo zingesaidia.
Sheikh Ponda amesema ahadi hiyo ya Rais ni ya kuungwa mkono kwa kuwa inaonyesha kujali masilahi ya wananchi, hususan Waislamu.
Juzi, akihutubia Baraza la Idd el Fitr jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema atawasaidia Waislamu kurejesha mali zao na kumpongeza Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Abubakar Zubeir kuwa alikuwa mstari wa mbele katika kurejesha mali hizo kabla hata hajapewa cheo hicho.
“Nakumbuka wakati nikiwa Waziri wa Ardhi, kabla hujawa Mufti, pamoja na viongozi wa Bakwata na wengine, ulifika ofisini kwangu ukieleza jinsi mali za Waislamu zilivyokuwa zinadhulumiwa.
"Ninafamu pamekuwa na hiyo tabia ya baadhi ya viongozi wenye mali kuwatumia viongozi wa Bakwata na dini nyingine katika kuwarubuni na kuingia ubia. Mali hizo baadaye huwa zinapotea kabisa,” alisema.
“Tujitahidi kwa nguvu zote kusimamia mali hizi zisije kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani. Tunapenda wawekezaji, lakini wanachokiahidi hawatekelezi. Haiwezekani.
“Haiwezekani na wala haikubaliki kwa watu kwa ujanja wao na wakati mwingine kwa kutumia wanasheria wao kukalia mali za Waislamu. Mali za Waislamu lazima zirudi na za Wakristo zirudi ili amani iwepo.”
Sheikh Ponda alisema kwa kauli hiyo, Rais Magufuli ametambua juhudi ambayo wamekuwa wakizifanya katika kupigania mali za Waislamu, kama ilivyokuwa katika kupigania kiwanja cha Chang’ombe hadi kusababisha kesi dhidi yake na wenzake.
“Utakumbuka, tulikuwa na kesi kuhusu kiwanja cha Waislamu kule Chang’ombe, katika hatua za awali tulishindwa, lakini baadaye tukakata rufaa na kushinda. Ndiyo sababu ya kuunga mkono kauli hii ya Rais,”alisema Sheikh Ponda.
Akizungumzia msaada wa Rais Magufuli kwa ajili ya Hija, alisema hiyo ni ruzuku muhimu, lakini Rais angekaa na Waislamu wamweleze mambo ambayo ni muhimu zaidi ili uwekezaji wake uwe na manufaa zaidi.
Alipoulizwa ni mambo gani ni muhimu zaidi, Sheikh Ponda alisema ni masuala ya elimu na afya ambayo Serikali ikisaidia baadaye yatapunguza mzigo mkubwa kwake
Post a Comment