Header Ads

Rais Magufuli Amwahidi kazi Meya wa UKAWA......Awamwagia Sifa Naibu Spika na Mchungaji Msigwa Kwa Kukaa Meza Moja

RAIS John Magufuli amemwahidi kwa utani kumpatia kazi Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, endapo atafukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kusifia kazi inayofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

Akizungumza na wageni waalikwa waliofika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana, kushuhudia shughuli ya makadhibiano ya madawati ambayo yalitokana na Sh. bilioni nne ambazo zilitolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ikiwa ni mpango wake wa kubana matumizi, Rais Magufuli alisema amekuwa akivutiwa na ‘statement’ (kauli) ambazo zimekuwa zikitolewa na meya huyo.

Alisema hata alipompatia nafasi ya kuwasalimia wananchi waliofika kwenye hafla hiyo, meya huyo aliongelea masuala muhimu yenye kuleta maendeleo kwa taifa.

Rais Magufuli alisema amekuwa akifuatilia kauli za Meya Mwita na kueleza hotuba zake zimekuwa zenye dhamira ya kuleta maendeleo.

Alisema kwa mzaha, ikiwa meya huyo atafukuzwa katika chama chake yeye atamkumbuka kwa sababu bado amebakiwa na nafasi nyingi za uteuzi.

“Ninafurahi Meya Mwita, ninakupongeza sana kwa sababu nimekuwa nikisikiliza sana `statement’ zako za maendeleo, sasa sijui nikisema hivi watakubakiza au watakufukuza, ila wakikufukuza mimi nitakukumbuka kwa sababu nina nafasi nyingi bado za uteuzi,” alisema Rais Magufuli kwa utani na kusababisha watu kucheka.

Alisema viongozi wanapaswa kulenga kutatua matatizo ya wananchi na siyo kuingiza masuala ya itikadi za vyama katika kila jambo.

Awasifu Dr Tulia na Mchungaji Msigwa
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwapongeza Mbunge wa Iringa (Chadema), Peter Msigwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Ackson Tulia, kwa kukaa pamoja katika meza kuu wakati wa hafla hiyo.

Wabunge kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walitangaza kususia vikao vya bunge vinavyoongozwa na Dk. Ackson au shughuli yoyote itakayoongozwa naye kwa madai amekuwa akiendesha vikao vya bunge kwa upendeleo na kutaka avuliwe wadhifa huo.

Rais Magufuli alisema inapofika masuala ya kuleta maendeleo ya taifa, viongozi wanapaswa kuweka kando masuala ya vyama.
 
Alisema hata yeye wakati akipiga kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, aliwaahidi Watanzania kuwa atawatumikia wote bila ya kuangalia vyama, kabila, dini wala rangi.

“Mmeacha vyama vyenu pembeni, mnaunga mkono maendeleo, leo unapomwona Msigwa na Tulia wapo jirani inatia moyo, ndicho tunachokitaka, nchi hii ni yetu sote, tukifanya hivyo nchi yetu itakuwa ya mfano,” alisema Rais Magufuli.

Alipoulizwa kwa kitendo chake cha kuhudhuria shughuli hiyo na kukaa meza moja na Dk, Ackson, Msigwa alisema wamefika katika hafla kama wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge.

Alisema pia walihudhuria hafla hiyo kwa sababu ni suala la maendeleo na walipaswa kushiriki ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama zilivyopangwa.

“Hii shughuli haiendeshwi wala kuandaliwa na Tulia, ni shughuli iliyoendeshwa na tume yetu na ndiyo maana tupo hapa,” alisema Msigwa.

Pia Rais Magufuli alimtaka Mbunge wa Kaliua(CUF), Magdalena Sakaya, kutoogopa kupeleka maendeleo katika jimbo lake kwa sababu maendeleo hayana chama

Mbunge huyo alisema hafla hiyo ni ya maendeleo hivyo hawakuwa na sababu ya wao kugomea.

Wabunge wa Ukawa waliwahi kukaririwa wakilalamikia kitendo cha uongozi wa Bunge kurejesha Sh. bilioni nne serikalini ili kubana matumizi.

Rais Magufuli, ambaye alikabidhiwa hundi ya fedha hizo Aprili 11, mwaka huu, alielekeza zitumike kutengeneza madawati, huku akizitaka ofisi na taasisi zingine za serikali kuiga mfano huo.

No comments