Header Ads

Mrema Ataka Watanzania Waupime Utendaji Kazi wake Baada ya Siku 100

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), Augustine Mrema amemmwagia sifa Rais John Magufuli huku akiwataka Watanzania kumpa siku 100 aonyeshe mabadiliko katika magereza nchini. 

Mrema aliyasema hayo jana alipohojiwa katika kipindi cha Amka Tuongee kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star tv.

“Ni Rais mzuri tuliyempata, ni mchapa kazi, tumpe muda kwa sababu ndiyo kwanza ana miezi minane, lakini ni mchapa kazi kiasi kwamba marais wenzake wanatembea yeye anakimbia,” alisema. 

Julai 16, Rais Magufuli alimteua Mrema ambaye ni Mwenyekiti TLP baada ya kumkumbusha ahadi aliyompa wakati wa kampeni eneo la Himo Kilimanjaro kuwa wasipomchagua kuwa Mbunge wa Vunjo atampatia kazi. 

“Nina uhakika nitafanikiwa kwa sababu nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani nilifanya mambo makubwa hadi nikapewa cheo cha Naibu Waziri Mkuu,” alisema.

No comments