Lori lakwepa magari manne, lagonga mengine manne na kuua watu wanne
Licha ya lori lililokosa breki katika Mlima Iwambi nje kidogo ya Jiji la Mbeya, kuyakwepa magari manne, limeyagonga mengine manne na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 22.
Ajali hiyo ilitokea juzi usiku katika mji mdogo wa Mbalizi, Barabara Kuu ya Mbeya - Tunduma, ambako lori hilo liligonga basi aina ya Toyota Coaster na magari madogo matatu.
Katika tukio hilo, watu watatu walifariki muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali Teule ya Ifisi na hadi tunakwenda mitamboni walikuwa hawajatambuliwa, huku mwingine aliyetambuliwa kwa jina Philip Cheyo (39) akifariki jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Ifisi, Elimate Sanga alisema walipokea miili ya watu watatu na majeruhi 22 wakiwamo sita waliohamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kutokana na hali zao kuwa mbaya. Sanga alisema hadi jana asubuhi, ali- kuwa na wagonjwa 12 waliolazwa.
Ofisa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa, Lucy Elias alisema Cheyo ambaye alikuwa mmoja wa majeruhi sita, alifariki jana asubuhi akiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari alisema wanachunguza chanzo cha ajali hiyo ingawa taarifa za awali zinaonyesha kuwa lori lilifeli breki wakati likiteremka mlima huo.
Akisimulia tukio hilo, kondakta wa lori hilo, Wilberd Joseph akiwa wodi ya nne ya Ifisi alisema lilianza kuongeza mwendo wakati wakianza kuteremka mlima huo na ndipo dereva akalalamika halina breki.
“Nilisikia dereva ananiambia, tuombe Mungu, breki zimegoma kabisa, ndipo lori likazidi kuchanganya na dereva alijitahidi kuyakwepa magari zaidi ya manne hivi, lakini tulipoingia mjini kabisa (Mbalizi), kulikuwa na (basi dogo) Hiace ikitokea upande wa kushoto kuingia barabara kuu, alipolikwepa tela likagonga basi jingine aina ya Coaster lililokuwa limesimama upande wa kulia,” alisema kondakta huyo.
Alisema baada ya kugonga basi hilo lililokuwa likitokea Tunduma kwenda Mbeya, pia liligonga magari mengine yaliyokuwa nyuma ya Coaster hiyo.
Mmoja wa majeruhi wa basi hilo, Isack Mwaipaja aliyelazwa katika Hospitali ya Ifisi, alisema walipofika Mbalizi dereva wao hakutaka kuingia stendi na aliamua kuteremsha abiria pembeni mwa barabara kuu ndipo ghafla wakasikia kishindo.
“Bila kujua kinachoendelea nikajiona nimelowa usoni, kupangusa hivi nikaona damu inavunja usoni, kumbe ni lori lilikuwa limetugonga ubavuni na wale waliokuwa nyuma ya basi ndiyo walioumia sana kwani tela lote liliishia huko,” alisema.
Post a Comment