HUU NDIO WARAKA UNAODAIWA KUANDIKWA NA JOHN MNYIKA KUMHUSU LOWASSA
Mtakumbuka ni muda sasa sijaonekana wala kusikika katika harakati za kisiasa. Leo nimependa kuweka bayana ili umma wa watanzania ufahamu kwani kumekuwa na upotoshwaji mkubwa juu ya ukimya wangu.
Napenda umma wa watanzania ufahamu yafuatayo:-
1. Msimamo wangu wa kuitaka serikali imkamate Mh Edward Lowassa, imhoji na imchukulie hatua kwa mujibu wa sheria kutokana na ushiriki wake katika kashfa ya RICHMOND haujabadilika kama ambavyo niliwahi kusema nikiwa mkurugenzi wa vijana wa CHADEMA tar 25 Februari 2008 na kipindi chote nikiwa Mbunge wa Ubungo.
Hivyo nategemea kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi Lowassa ndiyo atakuwa wa kwa. Siwezi kusaliti msimamo wangu bora nipoteze ubunge wangu.
2. Sikukubaliana na utaratibu uliotumika kumpata mgombea urais ndani ya Chama changu hususani ujio wa Mh Edward Lowassa mmoja wa watu ambao ni mizizi ya ufisadi hapa nchini. Hali hii ilinilazimu nikae kimya kutokana na kutokuamini kilichokuwa kinatokea hususani kwa Chama kama CHADEMA kilichojijenga na kujipatia umaarufu kwa kuongoza mapambamo dhidi ya rushwa, ubadhirifu, ufisadi na uwajibikaji mbovu wa serikali halafu tukasaliti msimamo wetu kwa uharaka wa kuipata dola! Sikukubaliana na sijakubaliana hata sasa.
3. Napenda kuzungumzia utendaji wa serikali ya Dkt Magufuli. Naomba Ifahamike nimekuwa mara zote nikisema matatizo ya msingi ya nchi yetu hayasababishwi na mapungufu ya sheria ila Kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na kulegea kwa misingi ya utawala wa sheria na uwajibikaji miongoni mwa viongozi. Hivyo kwa asilimia kubwa naona Dkt Magufuli ameweza kujibu nilichokuwa nikikilalamikia kwa muda sasa. Haya mengine yanazungumzika.
4. Sikubaliani pia na mtazamo wa baadhi ya viongozi wakiwemo wa Chama changu wanaotaka fedha za walipa kodi ziendelee kuteketea kwa ufisadi na ubadhirifu huku wahusika ambao ni wachache wakilindwa kwa kisingizio cha haki za binadamu. Kwa hili nampongeza Mh Rais kwa msimamo na hatua anazochukua japo apanue wigo ili watanzania maskini wanufaike na utajiri wa rasilimali walizojaliwa.
5. Vile vile naomba kuzungumzia mwenendo wetu kambi rasmi ya upinzani bungeni au UKAWA binafsi sifurahishwi na maagizo na maelekezo ya viongozi wetu juu ya kuingia na kutoka bungeni kwa hoja ambazo haziwagusi wananchi moja kwa moja kiasi cha kutufanya tushindwe kutimiza majukumu yetu kama wabunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) na (3) katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutunga sheria, kuisimamia serikali, kuwawakilisha wananchi na kupitisha mipango ya maendeleo. Sifurahishwi sababu kutoka Kwetu hakuna la msingi tunalofanya kwa ajili ya wananchi waliotutuma huko bungeni. Tusipobadilika itatugharimu!
Mwisho nawatakia waumini wote wa kiislamu mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Imetolewa leo tar 3 Julai 2016.
John Mnyika (Mb)
0754 694 553.
0754 694 553.
Note: Mbunge John Mnyika alipohojiwa kuhusu waraka huu, alisema kuwa siyo yeye aliyeandika na kuwa hafamu lolote kuhusu waraka huu.
Post a Comment