Header Ads

Chadema yawekewa ulinzi kila kona Dodoma ....Polisi watoa maagizo maalumu kwa wamiliki wa nyumba za wageni, Viongozi wa Bavicha wapandishwa kizimbani

Licha ya uongozi wa Chadema kutangaza kwamba umefuta mpango wa vijana wake (Bavicha), wa kuisaidia polisi kuzuia mkutano mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki ijayo, jeshi hilo limeimarisha ulinzi kila kona ya mji. 

Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Julai 23, utashuhudia Rais John Magufuli akipokea kijiti cha uenyekiti wa chama hicho kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya Kikwete. 

Kabla ya zuio la Mbowe, Bavicha walikuwa wameanza kujiandikisha katika maeneo mbalimbali na kuchangisha fedha kupata nauli ya kuja mjini Dodoma kuzuia mkutano huo huku polisi ikitangaza kupambana nao. 

Jana, polisi walifanya doria mji mzima wa Dodoma na kisha kukutana na wamiliki wa nyumba za wageni na kuwataka wageni wote watakaofika kwenye nyumba hizo kusajiliwa kwa vitambulisho vyao. 

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya kukamatwa kwa viongozi wa Bavicha ambao jana walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Dodoma kusomewa mashtaka na baadaye kuachiwa kwa dhamana wakidaiwa kukutwa na maandishi ya uchochezi kinyume na kifungu cha 32 (2) cha Sheria ya Magazeti, sura namba 229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. 

Waliofikishwa mahakamani ni Mwenyekiti wa Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Mkuu Julius Mwita, Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya, George Tito na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Joseph Kasambala. 

Akisoma mashtaka yao mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Lina Magoma alidai kuwa washtakiwa watatu; Katambi, Mwita na Tito walikutwa katika Baa ya Capetown mjini hapa Julai 8 wakiwa na fulana zilizoandikwa lugha ya uchochezi. 

Alinukuu maneno yaliyoandikwa katika fulana hizo kuwa ni “Mwalimu Nyerere: Demokrasia inanyongwa na Dikteta Uchwara.” 

Alisema upelelezi unaendelea na kwamba hakuwa na pingamizi na dhamana. Kasambala alifunguliwa jalada lake pekee licha ya shtaka lake kufanana na wenzake, tofauti ikiwa mahali alipokamatiwa na ujumbe huo kwenye fulana aliyokuwa ameivaa. 

Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana, Kasambala alisema mshtakiwa huyo alikutwa katika Kituo cha Polisi cha Kati Julai 9 akiwa amevaa fulana yenye maandishi; “Mwalimu Nyerere: Demokrasia inanyongwa.” Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na Hakimu Mfawidhi Karayemaha, aliwapa dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi hiyo itatajwa tena Julai 26 mahakamani hapo. 

Nje ya Mahakama 
Akizungumza na wanahabari nje ya mahakama hiyo, Katambi alisema tangu walipokamatwa Ijumaa iliyopita hawajawahi kuambiwa kosa lao. 

“Tulipokuwa Capetown tulipokwenda kula chakula walitokea askari waliovalia kiraia na kutuvuta nje wakituambia mkuu wao anahitaji kuzungumza na sisi lakini cha ajabu hawakutuambia kosa kwa muda wote tuliokaa ndani,” alisema. 

Alidai kuwa walihamishiwa katika rumande nyingine zilizopo Chamwino kutoka Kituo Kikuu cha Polisi bila kuwaambia ndugu, viongozi wa chama chao wala mawakili wanaowatetea. 

Alisema katika rumande hizo kila mshtakiwa alifungwa kwenye chumba chake. “... Sisi si majambazi lakini polisi wametumia nguvu kubwa kutukamata na kutushikilia bila sababu ya msingi. Lakini tuna imani Mahakama itatenda haki katika shauri hili.” 
 
Kuimarisha ulinzi 
Jana asubuhi, polisi waliokuwa wamebeba silaha za moto, mabomu ya machozi na mbwa walionekana wakizunguka kwa pikipiki na magari katika mitaa mbalimbali ya mji wa Dodoma. 

Msafara wa magari zaidi ya 20 likiwamo basi kubwa lililobeba askari na gari la maji ya kuwasha, lilizunguka katika mitaa mbalimbali kwa muda wa zaidi ya saa mbili. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema mara nyingi wamekuwa wakifanya mazoezi ya kutembea kwa miguu lakini wakati fulani huwa wanatumia vyombo ambavyo wamepewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao. 

“Leo tumetoka kistaili ambayo pengine haijazoeleka. Hatukuwa na matembezi ya miguu, tumetumia vyombo kwa maana ya pikipiki na magari yote tuliyonayo. Haya ni mazoezi ya kawaida mara nyingi tunafanya doria,” alisema.

Alisema doria hizo ni za pikipiki, miguu na magari na kwamba yote yaliyoonekana jana ni katika kuwajenga askari kuwa tayari kwa ajili ya kukabiliana na lolote litakalojitokeza akisema hayo ni mazoezi ya kawaida na kwamba waliojitokeza ni maofisa wa polisi, wakaguzi, askari wa vyeo vya juu na vya chini. 

Alisema aghalabu wanafanya mazoezi hayo usiku lakini kwa jana waliona wayafanye asubuhi ili kuwawezesha wakazi wa Dodoma kujivunia chombo chao cha polisi. 

Alipoulizwa kuhusu kauli za mitaani kuwa mazoezi hayo ni ishara kuwa wanaogopa vijana wa Chadema, Mambosasa alisema polisi hawaogopi mtu yeyote. 

“Kwanza ijulikane tunafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi, sheria, kanuni, mwongozo na taratibu zote zinazoongoza nchi. Kwa hiyo tunachokifanya si mambo mapya ni yale yaliyopo kisheria,” alisema. 

Alisema polisi hawaogopi wahalifu wa aina yoyote hata wa kutumia silaha na wamejipanga kukabiliana nao. 

“Na niwaambie tu... haogopwi mtu hapa, sisi tunasimamia sheria kwa kuwaelimisha watii sheria bila shuruti na wale wachache wasiotii tutawashurutisha,” alisema. 

Alisema wale wote wanaosema watafika Dodoma kulisaidia jeshi la polisi watawashurutisha kwa kutumia nguvu kidogo tu ili warudi kwenye mstari.

No comments