Ajali ya Lori Yaua Watatu Dodoma Wakitoka Mnadani
WATU watatu wamekufa baada ya kufukiwa na mizigo wakati lori walilokuwa wamepanda kutoka Mnada wa Mgaga wilayani Bahi mkoani Dodoma, kupasuka tairi na kupinduka.
Ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Chifutuka saa 11 jioni juzi, pia ilisababisha majeruhi 19 ambao wamekimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Mayala Towo alilitaja lori lililohusika kuwa ni aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 689 BEG.
Alisema lori hilo lilipofika eneo la Chifutuka wilayani Bahi, tairi lake la mbele lilichomoka na kupinduka.
“Gari hilo lilichomoka tairi ya mbele na kusababisha kupinduka kisha mizigo kuwaangukiwa watu waliokuwepo katika lori hilo ambapo watu watatu wamekufa na majeruhi 19 walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa,”alisema Towo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Zainabu Chaula alisema juzi saa mbili usiku walipokea majeruhi 19 na maiti watatu.
Dk Chaula alitaja waliokufa kuwa ni Isdori Thomas Motto (38), Michael Msongela (29) na Elias Masimo Petro (51) wote wakazi wa Dodoma.
Daktari huyo alisema majeruhi 12 walitibiwa na kuruhusiwa huku wengine wakilazwa wodi namba 10, 8 na 11 kwa ajili ya uangalizi zaidi.
Aliwataja waliolazwa kuwa ni Muoni Magege (40) mkazi wa Dar es Salaam, Suzy, Samweli (16), Frida Chipaga, Chausiku Mohammed (38), Josephine Sakiru (43), Selemani Salum (35) na Elias Petro (51) wote wakazi wa Dodoma.
Akisimulia ajali hiyo, mmoja wa majeruhi ambaye amelazwa katika Wodi Namba 8, Chausiku Mohammed mkazi wa Chinangali mjini Dodoma, alisema walipanda lori hilo lililokuwa likitoka mnadani na kwamba alichokiona ni kuchomoka kwa tairi la lori hilo, hivyo gari kupinduka na wao kufunikwa na mizigo iliyokuwepo katika lori hilo.
“Mimi nilienda mnadani kwa ajili ya kununua mazao, kama unavyojua malori ya minadani yanabeba kila kitu hadi mizigo sasa sisi kilichotuumiza ni mizigo kwani ilitulalia na mimi kama unavyoona nimeumia huu upande wote wa kulia na hapa katika mkono wangu,”alisema Chausiku.
Seleman Salum aliyelazwa Wodi Namba 11 mkazi wa Uwanja wa Ndege, alisema ajali hiyo ilisababishwa na kuchomoka kwa tairi la mbele na kupinduka. Alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11 jioni karibu na Kijiji cha Chifutuka wilayani Bahi.
Post a Comment