Polisi Dar es Salaam Wamng’ang’ania Zitto Kabwe
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema inaendelea na upelelezi kuhusu tuhuma zinazomkabili Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto ambaye ni Mbunge Kigoma Mjini na watakapokamilisha atafikishwa Mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema, sababu za kumhoji Zitto ni kutokana na kauli za uchochezi alizozitoa katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Zakhem, Mbagala.
Alisema, tayari Zitto ameshahojiwa katika kituo hicho mara mbili, lakini bado jeshi hilo linaendelea na upelelezi ili kujiridhisha dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Sirro alisema jeshi hilo haliwezi kuruhusu siasa ambazo zinavunja amani, hivyo ameendelea kuwataka wanasiasa kufuata taratibu na endapo wamekataza kufanya mikutano basi watii.
“Kama hakuna amani hakuna siasa hatuwezi na hatutakubali kuruhusu amani tuliyonayo itoweke sababu ya wanasiasa lazima kutii ili kulinda amani yetu,” alisema Sirro.
Hivi karibuni Zitto alijisalimisha Kituo cha Polisi na kuhojiwa kwa zaidi ya saa tatu baada ya kuandikiwa barua ya kuitwa kituoni na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camilius Wambura.
Hatua ya Zitto kuhojiwa ilitokana na maudhui ya hotuba yake aliyoitoa Juni 5, mwaka huu kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Zakhem, Mbagala wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kutoka katika mahojiano hayo, Zitto alisema haoni kama hotuba aliyoitoa ina tatizo lolote, kwani hotuba hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kisiasa.
Post a Comment