Header Ads

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Madiwani wanne Wafikishwa Mahakamani


MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na wenzake wanne ambao ni madiwani wa Halmashauri ya Meru wilayani Arumeru, wamesomewa shitaka la kuharibu uzio eneo la Leganga wilayani humo. 

Walisomewa shitaka lao mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augustine Rwezile jana.

Mwanasheria wa Serikali, Gaudensia Joseph alidai Nassari na wenzake ambao ni Paulo Samuel, Japhet Joseph, Zephania Mwanuo na Anderson Sikawa kwa pamoja na madiwani wenzao 24, ambao walisomewa shitaka lao awali waliharibu uzio wa Naftani Makere.

Joseph alimuomba Hakimu Rwezile kuwaongeza washtakiwa hao watano akiwemo Mbunge Nassari, ambapo awali katika shitaka lao linalowakabili mahakamani hapo, hawakuwepo mahakamani kwa sababu mbalimbali. Alidai wanashtakiwa kwa kuharibu uzio, Mei 4 mwaka huu, eneo la Leganga wilaya ya Meru.

Alidai walisababisha hasara ya Sh milioni 7 kwa kuharibu uzio huo. Wote walikana mashitaka. Mawakili wanaowatetea watuhumiwa hao ambao ni Charles Abraham na Gift Joshua, waliomba dhamana kwa wateja wao.

Hakimu Rwezile alikubali ombi la wakili huyo kutoa masharti ya dhamana ya kusaini Sh milioni moja na kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja. Walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana.

Washtakiwa wengine waliofikishwa awali ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meru, Willy Njau (Chadema) na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Nelson William. Wengine ni Elisa Stephen, Digna John, Dina Erick, Wilson Fanuel, Josephine Anael, Samuel Ismail, Agness Eliya, Isack Afitwe na Neema Isack.

Washtakiwa wengine ni Gadiel Stanley, Jeremiah Masawe, Peter Efatha, Benard Wilson, Henry Benjamin, Emanuel Pendael, Fadhila Joseph, Penzila Palangyo, Mary Antony, Roman Laurance, Bryson Mosses, Franck Ngoye na Eveline Julius. 

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 28 mwaka huu itakapotajwa tena kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

No comments