Wabunge EAC wampongeza Magufuli kutumbua majipu.
WABUNGE wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutoka Tanzania
wamesema hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli kutumbua majipu hasa
katika Bandari ya Dar es Salaam zimezipa matumaini nchi wanachama kuwa bandari
hiyo itafanya kazi zake kwa ufanisi.
Bandari ya Dar es Salaam imekuwa
ikitumiwa na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda kwa kupitisha mizigo yake kutoka
hapa nchini na Kenya.
Akizungumza jana na waandishi wa habari
mara baada ya kukutana na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mbunge wa Afrika
Mashariki, Shyrose Bhanji alisema Bunge la EAC lilishatoa pongezi kwa hatua
hiyo ya Rais Magufuli kutumbua majipu.
“Tumekuja hapa kwanza kumpongeza Spika
kwa kuchaguliwa, lakini pia kufikisha salamu zetu kutoka kwa Bunge la EAC kuwa
tumeridhishwa kwa kiasi kikubwa na kasi ya utendaji kazi wa Rais John
Magufuli,” alisema Shyrose.
Alisema, kutokana na kutumbuliwa majipu
hayo chini ya mfumo wa kufanya ziara za kushitukiza anazofanya, Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, umma wa Watanzania umetambua namna ambavyo baadhi ya watendaji
katika taasisi hiyo nyeti walikuwa wanafuja mali za umma.
Kuhusu Ndugai, Shyrose alisema, wabunge
hao ambao jimbo lao la uchaguzi ni Bunge la Tanzania, wameona vema kwenda
kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Spika mpya wa Bunge la 11.
Alisema, mwanasiasa huyo alistahili
nafasi hiyo kwa kuwa alifanya vizuri wakati akiwa Naibu Spika.
Aliongeza kuwa, pamoja na pongezi hizo,
wameona ipo haja ya mambo yanayojadiliwa ndani ya Bunge la EAC yawe
yanafikishwa pia kwenye Bunge la nchini kuwapa fursa wabunge kujua kinachoendelea
ndani ya jumuiya hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Habari Mkuu wa
Bunge, Owen Mwandumbe akizungumza kwa niaba ya Spika alisema, Ndugai
amewahakikishia kuwapa ushirikiano wa kutosha watekeleze majukumu yao kwa
ufanisi zaidi.
CREDIT:HABARI LEO
Post a Comment