Header Ads

Viongozi wa dini wahimizana kujitenga na siasa Zanzibar


VIONGOZI wa dini wa Tanzania Bara na Visiwani wamekutana visiwani Zanzibar na kuja na tamko juu ya hali ya amani visiwani humo ambalo pamoja na masuala mengine, wamehimizana kujitenga na siasa za vyama.

Aidha, viongozi hao kutoka madhehebu ya Kikristo, Kiislamu na Jumuiya ya Hindu wametaka wananchi watakaoshiriki kupiga kura katika uchaguzi wa marudio wahakikishiwe amani inatawala na wale ambao hawatashiriki, wasibughudhiwe na pia wahakikishiwe amani.

Pia wametaka vyama vya siasa vinavyotoa kauli na taarifa zisizo sahihi na hivyo kuleta uchochezi viache mwenendo huo ili kudumisha amani kwani kila mmoja ana wajibu wa kuitetea tunu hii ya taifa.

 Kikao cha viongozi hao kilifanyika juzi visiwani hapa chini ya Baraza la Viongozi wa Dini mbalimbali kwa Ujenzi wa Amani Tanzania (IRCPT).

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na baraza hilo, imetaja baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki kuwa ni Askofu wa Kanisa la Anglikana, Jimbo la Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Augustino Shao na Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum.

Wengine ni Askofu Dickson Kaganda; Shehe Norman Jongo ambaye ni mfanyakazi, Ofisi ya Mufti, Zanzibar; Shehe wa Tumbatu, Abdul Yusuf Mzee, Ismail Asahil na Godda Muyya ambaye ni Mwenyekiti wa Inter religious Peace Council, Tanzania 

Wakizungumzia hali halisi ya Zanzibar na nini kifanyike kudumisha amani, viongozi hao walisema viongozi wa dini wajitenge na siasa za vyama kwani wao wanapaswa kuwa nguzo za jamii zenye imani na asili tofauti, wasuluhishi na watetezi wa amani nchini.

Walisema wana mashaka kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwa jamii unaosababishwa na tofauti mbalimbali zikiwemo za kisiasa. 

Baada ya majadiliano ya kina, mambo mengine waliyoazimia ni kwamba, kwa kutambua kuwa Zanzibar ni moja na watu wake ni wamoja, amani ni tunu adhimu kwa Watanzania wote.

Waliwapongeza Wazanzibari kwa kuwa wavumilivu na kulinda amani katika kipindi cha kuanzia uchaguzi uliofutwa hadio sasa. Walitaka pia vyombo vya usalama wawabaini na kuwachukulia hatua vikundi vya uvunjifu wa amani ili wananchi waishi kwa amani.

Walivitaka vyombo husika kutumia nguvu inayostahili badala ya kuogopesha umma. Viongozi hao wa dini wameitaka Tume ya Uchaguzi kuwa waadilifu kusimamia haki, sheria, kanuni na uwazi kudumisha amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Vile vile wamevitaka vyombo vya habari kusaidia kuhakikisha nchi inapita kwenye uchaguzi kwa usalama na amani kwa kutoa taarifa sahihi, kuzingatia maadili na kufuata taratibu na sheria zilizopo.

No comments