Header Ads

Rais wa Vietnam Kutua Nchini Kesho Saa Mbili Usiku.


RAIS wa Vietnam, Truong Tan Sang anatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ziara rasmi ya kiserikali akifuatana na mke wake Mai Thi, mawaziri watano na wafanyabiashara 51. 

Hii ni ziara ya kwanza ya Mkuu wa nchi kuzuru nchini tangu Rais John Magufuli aingie Ikulu, lakini pia itakuwa ziara ya kwanza kwa Rais Truong kuzuru Afrika na Tanzania na baadaye ataelekea Msumbiji.

Pamoja na kuwa na mazungumzo na Rais Magufuli, Rais Truong atakutana na Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Spika wa Bunge Job Ndugai na kushiriki dhifa ya kitaifa Ikulu. 

Atakapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam saa 2.30 usiku kesho, Rais Truong atapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga.

Mapokezi rasmi kwa Rais huyo yatafanyika Jumatano Ikulu, Dar es Salaam ambapo kama zilivyo taratibu za kidiplomasia duniani, atapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi la Majeshi ya Ulinzi na Usalama. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Mahiga alisema baada ya kupokelewa Ikulu na Rais Magufuli, kupigiwa mizinga na kukagua gwaride, Rais Truong atakuwa na mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Rais Magufuli.

“Baada ya mazungumzo waheshimiwa marais watahudhuria hafla ya utiaji saini Mkataba wa masuala ya Kodi. Mkataba huu lengo lake ni kuchochea biashara baina ya Vietnam na Tanzania ambapo wafanyabiashara wa nchi zetu mbili hawatatozwa kodi mara mbili kwa biashara na uwekezaji watakaoufanya,” alisema Balozi Dk Mahiga. 

Alisema saa tano kesho, Rais Truong na ujumbe wake watakwenda katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba kwa ajili ya kukutana na Kikwete na kufanya mazungumzo, hasa kutokana na Rais Truong kuwa pia ni mmoja wa viongozi waandamizi wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam ambacho kina uhusiano wa muda mrefu na CCM.

Kwa kuzingatia mabadiliko makubwa katika uhusiano wa kimataifa ambapo dunia sasa inatupia macho zaidi kwenye diplomasia ya uchumi, baada ya kutoka Lumumba, Rais huyo atakwenda katika eneo maalumu la uwekezaji la EPZA Ubungo ambapo atapata fursa ya kutembelea viwanda na kupata taarifa za fursa za uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini.

“Saa 9:00 kamili jioni, Rais Truong na ujumbe wake watahudhuria Mkutano wa Biashara na Uwekezaji baina ya Vietnam na Tanzania.

"Saa 11 jioni atakutana na Spika wa Bunge Ndugai, saa 12.30 atakutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Shein na saa 1 jioni atahudhuria Dhifa ya Taifa, itakayoandaliwa kwa heshima yake na Rais Magufuli,” alisema Dk Mahiga.

Kwa mujibu wa Dk Mahiga, Alhamisi Machi 10, Rais Truong na ujumbe wake watakuwa na ratiba ya kutembelea mbuga za wanyama kati ya Saadani na Serengeti na Ijumaa Machi 11, Rais Truong na ujumbe wake wataondoka nchini kuelekea Msumbiji.

Katika ujumbe wake, Rais huyo atafuatana na mawaziri watano; wa Viwanda, Kilimo, Mawasiliano, Afya na Maji. 

Uhusiano wa Tanzania na Vietnam 
Balozi Mahiga alisema uhusiano wa Tanzania na Vietnam ulianza miaka ya 1960 wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati Vietnam ikiwa chini ya chama tawala cha Kikomunisti na Tanzania chini ya TANU (baadaye CCM) na kufanya kwa kiasi kikubwa nchi hizo kuwa na mambo yanayofanana kichama na kiserikali.

Alisema ikiwa nchi masikini kama Tanzania, Vietnam ilianzisha mapinduzi makubwa ya kuuhuisha uchumi wake ili kufikia uchumi wa kati, na katika miaka 15, uchumi wa nchi hiyo ulizaa miujiza, baada ya pato la mwananchi kutoka Dola 100 kwa mwaka hadi kufikia Dola 2,000 na kuwa mfano wa kuigwa kwa mataifa yanayoendelea Asia na Afrika. 

Ikiwa na ukubwa wa mita za mraba 330,000 ambao ni sawa na theluthi ya ukubwa wa Tanzania, ina idadi kubwa ya watu wanaofikia milioni 91 lakini Vietnam imefanikiwa kuwa nchi ya juu kabisa kwa uuzaji wa kahawa aina ya Robusta na korosho duniani na inaongoza kwa ufugaji wa samaki.

“Kinacholeta upekee hapa ni kwamba mbegu ya kahawa ya wa-Vietnam waliichukua hapa Tanzania mkoani Kagera, halafu mbegu ya korosho waliichukua Mtwara na mbegu ya samaki wanaotamba nao aina ya tilapia walichukua katika Ziwa Victoria,” anasema Waziri Mahiga.

Waziri Mahiga akizungumzia maendeleo katika mawasiliano anaitaja kampuni ya Viatel ambayo imepiga hatua kubwa ya mawasiliano duniani, Tanzania ikiendesha huduma zake kupitia mtandao wa mawasiliano wa Hallotel ambao ni maarufu zaidi katika maeneo ya vijijini kutokana na kutoa huduma za intaneti bure.

Vita ya Vietnam na Marekani 
Pengine jambo la haraka sana la kuwawezesha Watanzania kuifahamu Vietnam ni kuzungumzia vita ya Vietnam na Marekani, hasa kutokana na mabanda mengi yanayoonesha mikanda inayohusiana na vita jijini Dar es Salaam na katika miji mingi nchini kupenda zaidi kuonesha vita ya Vietnam na Marekani.

Chimbuko la vita ya Vietnam na Marekani, lilitokana na hatua ya nchi hiyo kugawanyika Kaskazini na Kusini mara baada ya Uhuru wake mwaka 1945, ambapo waasi wa Kusini walitaka kujitenga, hatua iliyosababisha serikali ya Kikomunisti kuamua kupigana ili kurejesha taifa moja.

Kutokana na kuzuka kwa vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe, Marekani iliamua kuingilia kati ili kuwasaidia waasi wa Vietnam Kusini wakijulikana zaidi kama Saigon, kabla ya kukumbana na kichapo kikali kutoka kwa Serikali ya Kikomunisti chini ya Jenerali maarufu Giap Nguyen huku askari wake 56,000 wakiuawa.

Waziri Mahiga alisema nidhamu, juhudi, maarifa na kutokubali kushindwa kama inavyoonesha katika mkanda huo wa vita, ndio chimbuko la mafanikio makubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo.

“Tunajifunza mambo matatu makubwa kutoka Vietnam; Moja uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii hata iwe katika mazingira magumu ikiwemo vita au amani. 

“Pili; ni watu wa utekelezaji na tatu ni uwezo wa kujibu swali; kwamba kama unataka kuendelea unahitaji nini, kwanza ni elimu ya ufundi, halafu miundombinu kama vile barabara, umeme, reli, maghala na mwisho mitaji ya kifedha, na hasa mapinduzi makubwa katika sekta ya benki ili kupata mikopo,” alisema Waziri Mahiga.

No comments