Header Ads

Magufuli apongezwa kutumia Kiswahili mikutano ya kimataifa


BARAZA la Kiswahili la Taifa (Bakita) limempongeza Rais John Magufuli kwa uzalendo wake wa kutumia Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Aidha, baraza hilo limesema katika kuhakikisha Kiswahili kinatumiwa vizuri, linaendelea kutekeleza mkakati wa kukamilisha kanuni zitakazopelekwa bungeni, kumwezesha Waziri mwenye dhamana kuwa na mamlaka ya kusimamia Sheria ya Lugha ya Kiswahili ya mwaka 1961, iliyorekebishwa mwaka 1985 kuipa nguvu ya kumshitaki mtu yeyote kwa matumizi mabaya ya lugha hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bakita, Profesa Martha Qorro alisema msimamo huo wa Rais Magufuli umesaidia Watanzania kupata taarifa moja kwa moja kutoka tukio husika.
“Uamuzi na msimamo wa Rais Magufuli wa kutumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa ikiwemo mkutano mkuu wa 17 wa viongozi wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokewa kwa furaha kubwa na wananchi na wadau wengi wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania,” alisema Profesa Martha.
Alisema kupitia msimamo huo, Bakita inaamini kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza lugha ya Kiswahili na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania kupitia tafsiri na ukalimani hivyo kuwezesha maendeleo kwa wananchi wote wa Afrika Mashariki.
Katibu Mtendaji wa Bakita, Dk Seleman Sewangi alitoa mwito kwa viongozi wengine wa ngazi mbalimbali za kitaifa kufuata nyao za rais kwa kuipa kipaumbele lugha ya Kiswahili kufikisha ujumbe kwa Watanzania walio wengi.
“Natoa mwito kwa viongozi wetu wa ngazi mbalimbali za kitaifa kutumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali za kitaifa na kuachana na dhana ya kutumia lugha ya kigeni yenye lengo la kuwafurahisha wageni wachache,” alisema Dk Sewangi.
Mkurugenzi,Taasisi ya Taaluma za Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ernesta Mosha, aliziomba ofisi za Serikali hususani mahakama, kutumia Kiswahili kwa kuwa ni lugha inayoeleweka na Watanzania wengi ikizingatiwa kuwa sio wote wanajua kutumia lugha ya kiingereza.
Akizungumzia kanuni, Dk Sewangi alisema zimetungwa na zitatumika kulinda matumizi ya lugha ya Kiswahili, lengo likiwa ni kusimamia matumizi ya lugha hiyo kwa usahihi na ufasaha. Alisema kanuni hizo ni kali na mtumiaji ama mchapishaji anayetumia kiswahili atakapokwenda kinyume, atachukuliwa hatua.
“Kanuni hazina muda mrefu kutoka, zinasubiri sheria ya Bakita ipite bungeni ambayo itawezesha kuruhusu kuwekwa kwa kipengelea cha kanuni hizo,” alisema Dk. Sewangi.

No comments