Header Ads

VIKUNDI VYA ULINZI SHIRIKISHI MARUFUKU DAR.


VIKUNDI vya Ulinzi Shirikishi katika Kituo Kikuu cha Polisi vimepigwa marufuku kutokana na malalamiko ya wananchi na utendaji mbovu wa kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema kuwa alifanya uchunguzi na kubaini mapungufu mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa vitendo vya rushwa.
Sirro alisema vikundi hivyo havifuati sheria na taratibu za ukamataji, ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kupita kiasi hata pasipohitajika.
‘’Kutokana na sababu nilizozitaja, nimesitisha vikundi hivyo kwa muda usiojulikana mpaka pale nitakapojiridhisha kuwa wamepata mafunzo maalumu ya ukamataji salama,’’ alisema Sirro.
Hata hivyo, alisema askari kanzu ndio watakaotumika kufanya operesheni ya kukamata pikipiki zinazovunja sheria za usalama barabarani na ukaguzi wa leseni za kuendeshea na za biashara.
Aidha, alitoa mwito kwa madereva wa bodaboda kuhakikisha kwamba wanakuwa na leseni za biashara zinazotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na leseni ya kuendeshea.
Aliwataka pia boda boda hao kufuata sheria za usalama barabarani kwani kwa kutofanya hivyo, watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Asilimia 90 ya bodaboda mjini hawana leseni za biashara, hivyo nawataka watafute leseni hizo ili kuwa na kibali cha kufanyia biashara,’’ alisisitiza.

No comments