Header Ads

Serikali yafyeka fedha za chakula kwa wabunge


Katika kile kinachoonekana kuwa ni mwendelezo wa Serikali ya awamu ya tano kubana matumizi, Bunge limepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha kwa ajili ya kuwanunulia chakula wabunge wakati wa vikao vya kamati mbalimbali za chombo hicho cha utungaji sheria, imefahamika.

Vyanzo vya uhakika vimeiambia Nipashe kuwa kuanzia sasa, Bunge litakuwa likiwapatia wabunge vitafunwa rahisi kama biskuti, sambusa na chai ambavyo kwa ujumla vitaigharimu ofisi ya Bunge si zaidi ya Sh. 10,000 tu kwa siku kwa kila mbunge, badala ya zaidi ya Sh. 30,000 zilizokuwa zikilipwa awali kumgharimia mbunge mmoja.

Kadhalika, Nipashe imebaini kuwa Bunge limefuta pia utaratibu wake wa kuwanunulia pipi wabunge ili kuchangamsha midomo wakati wa vikao vyao.

Chanzo cha uhakika kutoka Ofisi ya Bunge kimeiambia Nipashe kuwa kwa pamoja, hatua hizo zinatarajiwa kuokoa Sh. milioni 300 kwani kwa kila mwaka, vikao vya kamati za Bunge huketi walau wiki mbili katika kila mkutano wa Bunge na kwa mwaka, mikutano huwa ni minne.

Bunge la sasa ambalo ni la 11, lina kamati 18 zinazohusisha uongozi, kanuni na pia kamati za kusimamia sekta mbalimbali. Wajumbe wote kwa kila kamati ni 378, huku zaidi ya 50 kati yao wakiwa katika kamati mtambuka ambazo ni zaidi ya moja.

Imeelezwa kuwa kabla ya uamuzi mpya wa kubana matumizi ya fedha za chakula, wabunge walikuwa wakilishwa vyakula vya aina mbalimbali kila wanapokuwa kwenye vikao vyao vya kamati lakini sasa fedha hizo zimepunguzwa kwa kiasi kikubwa baada ya kuonekana ni matumizi yasiyo ya lazima kwani wabunge hulipwa pia mishahara na posho kwa ajili ya kutekeleza wajibu wao huo.

“Kabla ya uamuzi huu wa sasa chini ya mpango mpya wa serikali ya awamu ya tano wa kubana matumizi yasiyokuwa ya lazima, Ofisi ya Bunge ilikuwa ikitumia zaidi ya Sh. 30,000 kwa ajili ya kumlisha chakula kila mbunge katika vikao vyao vya kamati,” chanzo hicho kiliiambia Nipashe.

“Kwa kiwango hicho (Sh. 30,000), wabunge walikuwa na uhakika wa kulishwa vyakula vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na wali, nyama, kuku, ndizi, chapati, samaki, vinywaji na pia kupewa matunda," alisema mtoa habari wetu ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa sababu si msemaji rasmi.

"Lakini sasa vyakula hivyo havitakuwapo tena kwa sababu kiasi cha fedha kilichotengwa kimepunguzwa hadi kuwa chini ya Sh. 10,000 kwa kila mmoja.”

Chanzo hicho kiliiambia zaidi Nipashe kuwa kuna vitu vilikuwa vikiwekwa kwenye orodha ya vyakula havikuwa na msingi, na sasa vimepunguzwa kwa kiasi kikubwa ili kubana matumizi ya fedha za serikali.

Alipotafutwa ili kueleza undani wa taarifa hizo za kupunguzwa kwa fedha za chakula na pia kufutwa kwa ugawaji wa pipi kwa wabunge, Katibu Msaidizi wa Bunge - Uendeshaji, John Joel, alisema pipi kuondolewa bungeni siyo jambo la kuajabisha kwani huo ndiyo utaratibu wao mpya waliojiwekea.

"Mbunge anayehoji ni kwa nini pipi hazipo bungeni, muelezeni ni kanuni gani ambayo inawafanya wapewe pipi?" Alisema.

Kuhusu kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa fedha za chakula hadi kubaki vitafunwa pekee kutoka katika orodha ya vyakula mbalimbali walivyokuwa wakiwalisha wabunge wakati wa vikao vyao vya kamati, Joel alisema hana uhakika, lakini inawezekana jambo hilo likawa ni la kweli.

"Inawezekana ni kweli wakapunguza gharama, maana haiwezekani tuwalipe posho kila siku halafu bado tena tuwalipie na chakula wanapokuwa kwenye vikao vya kamati," alisema Joel ambaye alifafanua hata hivyo, "suala hilo halipo kwangu.

"Mtafute Mkurugenzi wa Utawala (wa Bunge) atakupa majibu mazuri."

Hata hivyo, alipotafutwa na mwandishi wa Nipashe ili kuelezea suala hilo, Mkurugenzi wa Utawala wa Bunge, alikataa kulitolea ufafanuzi.

NIDHAMU YA MATUMIZI, KUINUA MAPATO 
Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani baada ya kuapishwa Novemba 5 mwaka jana, serikali imekuwa mstari wa mbele katika kubana matumizi yasiyokuwa ya lazima na pia kuinua makusanyo ya kodi.

Lengo la mkakati huo, imeelezwa ni kuinua mapato na kuiwezesha kuboresha huduma za jamii kama afya, maji na pia kufanikisha mpango wake wa kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne kwa kila mtoto wa Tanzania.

Chini ya siku 100 za uongozi, tayari serikali ya Rais Magufuli imedhibiti mianya kadhaa ya matumizi yanayodaiwa kuwa siyo ya lazima, baadhi ikiwa ni kuzuia safari holela za viongozi na watumishi wa serikali kwenda nje ya nchi ambazo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na nusu ya 2014/2015, ziligharimu taifa zaidi ya Sh. bilioni 356.

Aidha, serikali imezuia matumizi ya fedha kwa ajili ya maadhimisho ya siku mbalimbali kama ‘wiki ya maji’ na ‘Siku ya Ukimwi Duniani’, kuzuia matumizi yatokanayo na uandaaji wa vikao vya kikazi kwenye kumbi binafsi na ulipaji wa posho kwa wajumbe wa vikao hivyo.

Aidha, serikali ilisitisha gwaride la sherehe za uhuru ambazo vinginevyo zingeligharimu taifa zaidi ya Sh. bilioni 4.

Kadhalika, watu kadhaa wamefikishwa mahakamani kutokana na tuhuma za ukwepaji kodi wa makontena yanayoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Wakuu wa taasisi mbalimbali wameondolewa katika nafasi zao au kusimamishwa ili kupisha uchunguzi kuhusiana na tuhuma mbalimbali za zinazohusiana na fedha za serikali.

Baadhi ya wakuu hao ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Awadh Massawe; aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), Rished Bade, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu.

Pia aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito ameondolewa kwa tuhuma kama hizo.

No comments