Header Ads

Sakata La Mauaji Ya Diwani Wa CUF Lachukua Sura Mpya.


Mauaji ya kikatili ya Diwani wa Kata ya Kimwani, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Sylvester Muliga (CUF), yameanza kuibua mambo mazito huku ikielezwa kuwa Ijumaa alikuwa awasilishe hoja kwenye Baraza la Madiwani kuhusu masuala ya ardhi.

Muliga ambaye alifia Hospitali ya Kagondo alikopelekwa kwa matibabu baada ya kukatwa mapanga Jumapili usiku, imeelezwa kuwa katika kikao hicho ilikuwa aombe kuundwa kwa kamati ya kuchunguza uhalali wa maeneo makubwa ya ardhi yanayomilikiwa na watu wachache.

Kwa mujibu wa mjumbe wa Kamati ya Uchumi na Mazingira ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kasharunga, Khalid Swalehe, hoja hiyo ilikuwa iwasilishwe na Muliga na ilikuwa inaungwa mkono na madiwani wa kata zote zilizo na migogoro ya ardhi.

Baada ya taarifa za kufariki dunia kwa diwani huyo, wananchi walivamia nyumba nane za watuhumiwa wanaodaiwa kutekeleza mauaji hayo na kuziteketeza kwa moto.

Pia, walichoma moto mashine mbili za kusaga na kuharibu gari la mmoja wa wagombea wa udiwani katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kyota, Daudi Kiruma, wananchi wamehusisha mauaji hayo na mambo ya siasa.

“Kinachoonekana hapa baadhi ya watu wanataka kupotosha ajenda ili wahusika wa mauaji wapate nafasi ya kutoroka,” alisema Kiruma.

Hata hivyo, Kiruma alisema hana uhakika kama mtuhumiwa anayedaiwa alikuwa mgombea amekamatwa, kwa sababu haonekani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, jana alisema wanamshikilia mtuhumiwa mwingine ambaye anafanya idadi ya walikomatwa kuhusiana na mauaji hayo kufikia watatu mpaka sasa.

Kamanda Ollomi aliwataka wananchi wasijadili mauaji hayo kwa hisia za kisiasa bali waviachie vyombo vya dola vifanye kazi yake.

No comments