Header Ads

Hakuna uvamizi Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef.

SERIKALI imesema Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef wa mkoani Geita, upo salama na hakuna uvamizi wowote uliofanywa na wachimbaji wadogo katika maeneo ya mgodi huo.
Katika hatua nyingine, imerejea mwito wake wa kutaka uongozi wa mgodi huo kuanza uzalishaji mara moja kama ilivyoagizwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alipotembelea mgodi huo hivi karibuni.
Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud amesema hayo akijibu tuhuma zilizotolewa na Kampuni ya Tanzam2000 inayomiliki mgodi huo kwa ubia na Shirika la Taifa la Madini (Stamico), kuwa maeneo ya mgodi huo yamevamiwa na wachimbaji wadogo baada ya kupata baraka za serikali kupitia kwa Naibu Waziri.
Kwa mujibu wa taarifa ya Masoud, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Royalty Exploration alitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kusambaza pia kwenye masoko ya hisa akilalamikia kuvunjwa kwa sheria za uwekezaji kwa kile alichodai kuwa wachimbaji wadogo walikuwa wamevamia maeneo ya mgodi huo isivyo halali.
“Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa uvamizi huo ulikuwa umeelekezwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini wakati alipoutembelea mgodi huo hivi karibuni. Kwa bahati mbaya sana taarifa hiyo ilikuwa na mambo mengi ambayo si sahihi na zenye lengo la kuchafua hadhi ya Naibu Waziri, Serikali ya Tanzania na Watanzania kwamba hawazingatii utawala wa kisheria na wanakiuka mkataba wa uwekezaji.”
Kwa mujibu wa Masoud, pamoja na kutokuwepo kwa lengo la serikali la kuingilia mkataba wa makubaliano ya uendeshaji wa mgodi huo baina ya Stamico na Tanzam, lakini serikali hairidhishwi na maendeleo ya uendeshaji wa mgodi huo na ndiyo ulikuwa ujumbe mkuu wa Naibu Waziri wakati alipoutembelea Mgodi wa Buckreef.

CHANZO:HABARI LEO

No comments