Header Ads

Wizi wa dawa hospitalini waitesa serikali.

Serikali kupitia Wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia watoto na wazee  imesema  kati ya asilimia 70 ya dawa zinazotolewa na serikali kwenda kwenye hospitali na vituo vya afya  ni asilimia 30 pekee huwafikia walengwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa wizara hiyo Ummy Mwalimu wakati wa ziara ya makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan  alipokua akizindua jengo la wagonjwa wa dharula katika hospitali  teule ya rufaa ya Mkoa wa Geita.

Waziri Mwalimu alisema serikali imekuwa ikijitahidi kutoa dawa mahospitalini lakini kutokana  na wizi unaofanywa na watumishi wasio waaminifu ni asilimia 30 pekee ndio huwafikia wagonjwa huku asilimia 40 ikiuzwa kinyemela.

Alisema serikali ya awamu ya tano haitaendelea kufumbia macho jambo hilo na wizara yake haitawavumilia watumishi  wasio waadilifu  wanaopokea dawa na kuziuza huku wananchi wakiilamu serikali kuwa haiwajali.

Mwalimu alisema katika kukabiliana na wizi huo serikali tayari imeweka alama maalum ambapo mtu yeyote atakaekamatwa akiuza dawa zenye alama ya serikali ataisaidia serikali kujua alikozipata lakini pia amewaagiza  watu wa bohari ya dawa (MSD) kutokushusha dawa kwenye vituo vya afya kama kamati ya afya haipo kwenye eneo hilo.

Aidha aliwataka wananchi kushirikiana na serikali kufichua wizi unaofanywa na watumishi wasiowaaminifu kwa kutoa siri pale watakaponunua dawa madukani zenye alama ya serikali ili sheria iweze kuchukuliwa .

No comments