Header Ads

Polisi mkoani Mwanza yakanusha kuhusika na uhalifu.


 Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Polisi mkoani Mwanza imekanusha kuhusika na uhalifu kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini.

Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justus Kamugisha alipokuwa akizungumza ofisini kwake kuhusu tuhuma zilizotolewa juu ya Jeshi la Polisi mkoani humo kuhusika na Uhalifu.

Kamanda Justus Kamugisha amesema kuwa kuna taarifa zimekuwa zikitolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Jeshi la polisi mkoani humo linajihusisha na masuala ya uhalifu ikiwemo baadhi ya maofisa wao kushirikiana na wahalifu katika uuzaji wa dawa za kulevya pamoja na kushirikiana na majambazi kupora mali za wananchi .

“Ni habari za uongo na za kulichafua Jeshi la Polisi na mimi kama Kamanda wa Polisi nimelipokea suala hili kwa masikitiko na natoa onyo kwa vyombo vya habari na jamii kwa ujumla kuacha tabia ya kueneza habari sizizokuwa za kweli” Amesema Kamanda Kamugisha.

Aidha Kamanda Kamugisha amesema kuna malalamiko yanayotolewa kuhusu Jeshi la Polisi mkoani hapo kujihusisha na ulanguzi wa bidhaa zinazouzwa kwenye kanteeni za Polisi, taarifa hizo ni za uongo kwani Serikali imeshafuta msamaha wa kodi katika bidhaa hizo ambazo zilikuwa na bei tofauti na zile zilizopo katika maduka ya kiraia.

Jeshi la Polisi ni chombo cha ulinzi na usalama wa raia na mali zake hivyo wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kupamabana na uhalifu uliopo.
CHANZO:MPEKUZI

No comments