Nape Nauye Asema TBC Haitarusha 'Live' Matukio Ya Bunge Kuanzia Leo ili Kubana Matumizi.
MWENYEKITI wa Bunge, Andrew Chenge leo ameahirisha bunge mara mbili kutokana na mvutano ulioibuka baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuomba bunge liahirishe kujadili hotuba ya rais na badala yake wajadili kuzuiwa kwa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC) kurusha matangazo ya moja kwa moja.
Kabla ya kuahirishwa kwa bunge, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliwasilisha taarifa ya serikali kulieleza bunge kwamba, serikali imesitisha huduma ya matangazo ya moja kwa moja kupitia TBC.
Kutokana na taarifa hiyo, Zitto alisimama na kuliomba bunge kusitisha shughuli za kuendelea kujadili hotuba ya rais ambayo ilianza kujadiliwa jana ili kutoa fursa kujadiliwa hatua ya serikali kuzuia haki ya wananchi kupata matangazao ya moja kwa moja kupitia televisheni hiyo.
Hata hivyo, Chenge alianza kuonesha nia ya kutaka kuzima hoja ya Zitto lakini wabunge wa upinzani kwa umoja wao waliungana na Zitto katika kushikilia msimamo wa kujadiliwa suala la TBC kabla ya kuendelea na mjadala wa hotuba ya rais.
Yalisikika maneno kama ‘usituburuze, mtemi, hapa hakuna kuburuzana’ huku wabunge wengine wakipiga kelele kuashiria kuunga mkono hoja ya Zitto.
Kutokana na mvutano huo, Chenge alilazimika kuagiza kamati ya uongozi kukutana ili kujadili taarifa hiyo na baadaye kuwasilisha kulichojadiliwa na kamati hiyo.
“Naipa kamati saa moja,” alisema Chenge jambo ambalo lilipokelewa kwa mikono miwili na upinzani. Baada ya kauli hiyo mwenyekiti huyo aliahirisha bunge kwa saa moja.
Hata hivyo, baada ya bunge hilo kurejea tena baada ya kupita saa moja , Chenge aliahirisha tena bunge kwa kuwa, kamati ilikuwa haijamaliza kujadili.
Wakati akizungumza bungeni wakati wa kuwasilisha kauli ya serikali Nape alisema, “naomba kutoa kauli ya serikali kuhusu TBC kutangaza moja kwa moja vikao vya majadiliano ya bunge.”
TBC ilianza kurusha moja kwa moja matangazo ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005. Kabla ya kuanza kurusha moja kwa moja, TBC wakati huo televisheni ya taifa ilikuwa inarekodi matukio yote ya bunge na kurusha usiku katika vipindi maalumu vilivyojulikana kama bungeni leo kwa maana ya yaliyojiri ndani ya bunge kwa siku husika.
Hata hivyo Nape alisema “baada ya kuanza kwa utaratibu wa kuanza kurusha matangazo moja kwa moja mwaka 2005, gharama za kufanya kazi hio zimekua zikipanda kwa kasi hadi kufikia Sh. 4.2 bilioni kwa mwaka kwa maana ya mikutano minne ya bunge.
“Shirika limekuwa likigharamia kwa sehemu kubwa matangazo hayo kwa kutumia mapato yake yanayotokana na matangazo madogo madogo ya biashara, ifahamike kuwa asilimia 75 ni vipindi vingi vinavyolenga kutoa elimu kwa umma na asilimia 25 ni burudani.”
Nape amesema, kutokana na hali hii, TBC imeona ni busara kubadilisha mfumo wa utangazaji wa shughuli za bunge ili kukabiliana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.
Amesema TBC imeona ni busara kuanzia mkutano huu wa bunge iwe inarusha baadhi ya matangazo ya bunge moja kwa moja yaani ‘live’ ikiwa ni njia ya kubana matumizi.
Amefafanua kuwa, “chini ya utaratibu huu, TBC itahakikisha kuwa, baadhi ya matukio ya matukio ya bunge yatarushwa moja kwa moja na mengine kurekodiwa na kuandaliwa kipindi maalum kitakachoitwa leo katika bunge.
“Kipindi hiki kitakua na mambo yote muhimu yaliyojiri ndani ya bunge kwa siku husika. Kipindi hichi kitakuwa kinarushwa kuanzia saa nne usiku hadi saa tano usiku.”
Post a Comment