Header Ads

Mkurugenzi Bariadi atumbuliwa `jipu`

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Bariadi, Erica Mussika, amesimamishwa kazi kwa kushindwa kusimamia mradi wa barabara wa Sh. Bilioni 9.192 uliokuwa ukitekelezwa katika mji huo.

Mbali na Mkurugenzi huyo, mhandisi wa ujenzi wa wilaya, Ruben Muyungi naye amesimamishwa kwa tatuzi hilo.

Walibainika kushindwa kusimamia vizuri mradi wa mkopo nafuu wa Benki ya Dunia ambao uliainisha kujenga barabara ya urefu wa kilomita 4.5 kwa kiwango cha lami, ndani ya mji huo.

Katibu mkuu wa Tamisemi, Musa Iyombe, alisema uamuzi huo umechukuliwa na Rais John Magufuli, baada ya kukasirishwa na kitendo cha watu wachache kutumia rasilimali za serikali vibaya na kuwanufaisha watu wachache.

Iyombe alisema mbali na kusimamishwa kwa mkurugenzi huyo, Rais Magufuli amefuta kibali chake cha safari ya kwenda Japan katika mafunzo, akimtaka mara moja kurejea kituo chake cha kazi ili kushirikiana na Takukuru kuona mradi huo kama umehusishwa na vitendo vya rushwa.

Aidha, Iyombe alisema mhandisi Muyungi aliyehamishiwa mkoa wa Manyara, amefukuzwa kazi na kuamuriwa kukamatwa na kuletwa wilayani Bariadi ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.

Sambamba na hilo, katibu mkuu huyo ameiagiza bodi ya wahandisi nchini kuchunguza kwa kina na kumfutia hati ya uhandisi kwa kushindwa kutumia taaluma yake vizuri na kusababisha baadhi ya barabara zilizojengwa katika mji huo kurudiwa mara mara kwa kuwekwa viraka.

Aidha, Katibu mkuu wa Tamisemi, Iyombe alimuangiza msimamizi mkuu wa mkandarasi wa kampuni ya Jasco inayojenga barabara hiyo ya kilomita 4.5 kwa kiwango cha lami, kumueleza kuwa utendaji wake wa kazi hauridhishi na kuhakikisha bodi ya wakandarasi inamchukulia hatua kali kwa kukiuka taratibu za ukandarasi.

No comments