Header Ads

Miundombinu kikwazo sekta ya utalii nchini

Ukosefu wa miundombinu katika baadhi ya mikoa yenye vivutio vya utalii umetajwa kuwa kikwazo kwa watalii kufika maeneo hayo na kusababisha kukosekana kwa mapato.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mkurugenzi mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devotha Mdachi alisema Serikali inapaswa kufanya juhudi za makusudi za kuboresha miundombinu katika mikoa yenye vitutio hivyo, hasa Kigoma.

“TTB tuna jukumu la kuhakikisha tunaongeza kiwango cha idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka milioni 1.5 kwa mwaka hadi kufikia milioni 3. Uwezo wa kufikia idadi hiyo tunao, isipokuwa kuna vikwazo kadhaa ambavyo Serikali inapaswa kutusaidia ili tufikie lengo,” alisema Mdachi.

Alisema Kigoma ni miongoni mwa maeneo yenye kero ya usafiri licha ya kuwa kuna Ziwa Tanganyika ambalo watalii wengi hupenda kwenda kuliona na wengine kutaka kuvua.

“Lakini pia kuna sokwe kwenye hifadhi ya Mahale na Gombe na ni eneo la kihitostoria, Livingstone aliwahi kuishi huko,” alisema Mdachi.

Alisema kwa sasa watalii wanaopenda kwenda huko hulazimika kutumia usafiri wa treni ambao huchukua muda mrefu njiani tofauti na maeneo ya vivutio vilivyopo katika mikoa ya kaskazini iliyo na  uhakika wa usafiri wa ndege.

Hata hivyo, alisema kuna malalamiko mengi kutoka kwa watalii yanayopaswa kufanyiwa kazi na Serikali.

Alisema wengi wao wanalalamikia kutoridhishwa na huduma za malazi zinazotolewa na baadhi ya hoteli wanazofikia hapa nchini, wakilinganisha na nchi nyingine.

“Kuna baadhi ya wamiliki wa hoteli huajiri watu wasiokuwa na sifa, wengi wao wanashindwa kutoa huduma kwa wateja wao kwa kiwango kinachotarajiwa,” alisema Mdachi.

Mkurugenzi huyo alisema ufinyu wa bajeti ya matangazo katika sekta ya utalii, pia ni kikwazo katika utendaji.

No comments