Maalim Seif Sharif Hamad Amwandikia Barua Papa Francis Kumwomba Aingilie Kati Mzozo wa Zazibar
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, amemwangukia Papa Francis kwa kumwandikia barua, akimuomba kutumia ushawishi wake na Tanzania kumaliza mzozo wa kisiasa kisiwani humo kabla hali haijawa mbaya.
Kwa mujibu wa barua yake ya Novemba 25, mwaka jana, Maalim Seif alimwomba Papa kutumia ushawishi alionao kwa serikali ya Tanzania ili kuhakikisha haki inatendeka na kuepusha vurugu zinazoweza kutokea.
“Ni wiki tatu sasa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu na hali hii imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kuichumi kutokana na wananchi wengi kuwa na hofu kuhusu mustakabali wa hali hii….watu wanashindwa kujua nini kitatokea maana wana hofu kwamba hali hii inaweza kuharibu umoja wa kitaifa kwa watu kuishi kwa upendo bila kujali dini wala kabila,” ilisema barua hiyo.
Barua hiyo ya Maalim Seif ilisema, Zanzibar ina mchanganyiko wa Waislamu na Wakristo, hivyo hakuna mgawanyiko kwa misingi ya udini lakini hatua ya wananchi kukosa haki yao ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura baada ya miaka 20 ya chaguzi visiwani humo kunaweza kusababisha vijana ambao hawafurahishwi na mwenendo huo kutumia njia mbaya kutafuta haki yao.
“Badala ya kuchukua hatua za pamoja kuzuia uovu huu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo chama chake kilishinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita, imekuwa ikisaidia serikali ya Zanzibar kwa kutumia askari na majeshi yake kutishia watu wa upinzani,”ilisema.
“Wakati mmishenari wa kikristu alipomuomba Sultan wa Zanzibar mwaka 1840 kibali cha kujenga asasi ya kusaidia jamii kwenye eneo lake, Sultani yule ambaye alikuwa Muislamu alimtambua kama mtumishi wa Mungu aliyekuwa na lengo la kuendeleza neno la Mungu” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Papa.
Iliongeza kuwa, Zanzibar ilipopata Uhuru wake mwaka 1963, kwa kiwango kikubwa watu wake waliishi kwa amani na ushirikiano baina ya watu wa madhehebu yote ya Katoliki, Anglikana, Sunni, Shia na Hindu na hakukuwahi kuwa na mgogoro wala hofu ya watu hao kuhitilafiana kwa misingi ya tofauti ya dini.
Ilisema Chama cha Wananchi CUF kimekuwa kikishinda chaguzi zote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, lakini haijawahi kupewa ushindi wake hata muhula mmoja.
CREDIT:MPEKUZI
Post a Comment