Header Ads

Benard Membe Akaribishwa CHADEMA.


Waziri wa zamani wa Mamboya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amekaribishwa kujiunga na Chama Cga Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ikiwa ni siku chache tangu atoe maoni yake akiikosoa serikali ya Rais John Magufuli.

Mwanasiasa huyo mkongwe amekaribishwa na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob ambaye alimshawishi kwa kutumia mifano ya wanasiasa wakongwe waliokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliohamia Chadema na Ukawa kwa ujumla akiwemo Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Kingunge Ngombale Mwiru.

Wiki iliyopita Membe alinukuliwa akimkosoa Dk Magufuli katika maeneo kadhaa, likiwamo la kubana matumizi, kudhibiti safari za nje na uteuzi wa Baraza la Mawaziri.

Jana, meya huyo kutoka Chadema alisema watu wanamshangaa Membe na kumshambulia siyo kwa sababu amesema mambo ya ajabu, ila yeye si mtu sahihi wa kutoa kauli hiyo.

“Watu hawashangai alichosema (Membe) kwa sababu siyo hoja ngeni, zimesemwa sana na wapinzani. Wanachoshangaa ni yeye (Membe) kusema hayo. Hafanani na hoja anazoziongea,” alisema.

Jacob ambaye alikuwa diwani katika manispaa hiyo katika Serikali ya Awamu ya Nne alisema, hoja zilizotolewa na Membe ni nzuri na kama zingetolewa na mpinzani zingeonekana zina mashiko zaidi.

"Asiwe vuguvugu, hicho ndicho kinachompa shida. Kama anataka kuja huku asiwe na wasiwasi chama changu kitampokea na hata hayo anayoyaongea yatakuwa na mantiki na watu watamsikiliza kwa sababu ni upinzani,” alisema na kuongeza;

“Avuke moja kwa moja kama walivyofanya akina Kingunge (Ngombale Mwiru), (Edward) Lowassa, na (Frederick) Sumaye kuhamia upinzani.”

Jacob alisema Sumaye na Lowassa ambao waliwahi kuwa mawaziri wakuu na Kingunge aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, walikuwa viongozi wa ngazi za juu, lakini walihamia upande wa pili (upinzani) na sasa wanaisimamia na kuikosa Serikali kwa uhuru.

“Asiwe mwoga kwamba ataishi maisha gani, Sumaye na Lowassa wamekuwa mawaziri wakuu wakaondoka na maisha yanaendelea.”

Hata hivyo, Jacob alisema Membe hakupaswa kukosoa sera ya Rais Magufuli ya matumizi na Rais kudhibiti safari za nje, kwa sababu yeye amenufaika nayo.

“Nadhani hakuwa mtu sahihi kusema hayo, alipaswa kwanza kumtafuta mtu mwingine aseme halafu yeye afuate baadaye, lakini kuanza kusema yeye moja kwa moja wakati alikuwa ananufaika na anachopinga Rais, anaonekana anamwonea wivu na mgongano wa masilahi.

“Sasa anapoanza yeye kujibu inashangaza. Kwa sababu yeye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, iliyokuwa inafanya matumizi makubwa halafu unakosoa unaonekana kabisa unaonyesha kuna mgongano wa masilahi,” alisema na kuongeza:

Jacob alisema kwa mpinzani kusema hivyo angeonekana anataka kumuwajibisha Rais ili hayo mambo yaangaliwe kwa kina zaidi.

Alitoa mfano wa waziri wa zamani, Dk Makongoro Mahanga na kusema alipoikosa Serikali hakushambuliwa kwa sababu alishahama kutoka CCM na sasa yupo upinzani.

“Alipozungumzia suala la matumizi ya ardhi, Serikali haikujibu ilikaa kimya kwa sababu aliyeongea ni mtu sahihi,” alisema na kuongeza.

" Kwanza alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri na pili hivi sasa yupo kwenye upande wa kuishambulia na kuikosoa Serikali na kuiwajibisha.”

No comments